Dar es Salaam. Asiye bahati habahatiki, wahenga walisema. Msemo huu unadhihirika katika Kijiji cha Ndumbi ambacho hakina bomba, lakini maji ya Ziwa Nyasa mkoani Ruvuma kinachotegemea, vipimo vinaonyesha yana sumu ya zebaki ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu.
Wananchi wa kijiji hicho kilichopo zaidi ya kilomita 90 kutoka barabara kuu itokayo Songea kwenda Mbinga hufanya shughuli zao kwa kutegemea maji ya ziwani.
Ingawa huo ndio mfumo wao wa maisha kwa muda mrefu, hali inakuwa tete baada ya vipimo vya mkemia mkuu wa Serikali kubaini kuwapo kwa kiasi kikubwa cha zebaki kutokana na shughuli za uchimbaji na usafirishaji mkaa wa mawe.
Wingi wa chembechembe za zebaki katika kijiji hicho unaelezwa kusababishwa na usafirishaji wa mkaa unaochimbwa katika Mgodi wa Ngaka kuelekea jijini Mbeya au nchini jirani, Malawi.
Vipimo hivyo vya maabara vinaonyesha kiwango cha zebaki katika Bandari ya Ndumbi kimezidi mara tatu ya kile cha kawaida hali inayotishia ustawi wa viumbehai wakiwamo wakazi wa eneo hilo.
Vipimo hivyo vya mkemia mkuu vilifanywa kutokana na ombi la Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc) lililokuwa linaandaa ripoti ijulikanayo kama ‘Monitoring and Inspection Report for Tunduru, Mbinga and Nyasa Districts.’
“Ndumbi ni bandari ndogo inayoendelea kujengwa. Kwenye ukaguzi wetu, watalaamu walikuta mrundikano na vipande vya mkaa wa mawe vilivyotapakaa ardhini na vingine kusombwa na maji kuingia ziwani. Hapakuwa na jitihada zozote za kulinda mazingira hivyo kusababisha uchafuzi wa maji bandarini hapo,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Matokeo ya vipimo vilivyochukuliwa na mkemia mkuu katika Bandari ya Ndumbi, ripoti inasema kiasi cha zebaki kilikuwa zaidi ya mara tatu ya kinachoshauriwa.
“Tumekuta kuna miligramu 0.018 za zebaki katika kila lita moja tofauti na miligramu 0.005 zinazokubalika. Jirani na ziwa kuna lundo la mkaa wa mawe ambao husombwa mvua ikinyesha. Huenda ikawa imesababisha ongezeko hilo la zebaki,” inasomeka ripoti hiyo.
Mratibu wa programu ya taka za hospitalini wa Wizara ya Afya, Honest Anicetus anasema Serikali inachukua hatua kupunguza madhara yatokanayo na kusambaa kwa madini ya zebaki kutokana na huduma zinazotolewa hospitalini.
Anasema hakuna namna nzuri zaidi ya kuyaepuka maeneo yaliyoathirika na sumu ya madini hayo.
“Upo mpango wa kupunguza vifaatiba vyenye zebaki kama vile themomita, vipimo vya presha na mashine za kuzibia meno. Ni mpango wa miaka minne unaoisha mwaka 2020,” anasema Anicetus.
Hata hivyo, wananchi hawajui maji wanayoyategemea ni hatari.
Naibu meneja wa Mgodi wa Ngaka, Edward Mwanga anasema walipopewa ripoti na Nemc kuhusu maji ya bandarini hapo, kwanza walishangaa lakini wakachukua hatua.
“Tumesitisha shughuli zote pale ili kupunguza madhara kwa wananchi. Tumefukia mabwawa yaliyokuwa yanatuamisha maji. Tunakusudia kufanya vipimo vingine kabla ya kuwajuza wananchi na wadau wengine,” anasema Mwanga.
Haja ya kuyapima tena maji hayo anasema inatokana na zebaki kugundulika Ndumbi pekee lakini Ngaka yanapochimbwa au Amani Makolo, kituo cha mauzo na usafirishaji kwa kutumia malori hakukuwa na zebaki.
Mkurugenzi mkuu wa Nemc, Dk Samuel Gwamaka anasema mgodi unapaswa kuchukua hatua zote muhimu kuhakikisha wananchi hawaathiriki.
“Tutaenda kuona ufukiaji walioufanya kama unakidhi maelekezo,” anasema Dk Gwamaka.
Licha ya hatua zilizochukuliwa, Mwanga anasema usafirishaji wa mkaa kupitia bandari ulisitishwa tangu mwaka 2014 kutokana na meli (burg) waliyokuwa wanaitumia kuwa chakavu.
Ofisa afya na usalama kazini wa mgodi huo, Emmanuel Charles anasema uchunguzi zaidi unahitajika kwa sababu mchanganyiko wa mkaa na maji hauwezi kuzalisha zebaki.
“Mkaa na maji huzalisha ‘sulphuric acid.’ Hapa mgodini tunayo mabwawa ya kuhakikisha asidi hii haitiririki kwenye vyanzo vya maji wanayotumia wananchi. Yakiwa mengi, tunayachanganya na chokaa kuondoa sumu hiyo,” anasema Charles.
Wadau
Mjiolojia na mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Dk Elisante Mshiu anasema tofauti na sumu nyingine, zebaki huwa haitoki mwilini endapo mtu atakunywa maji au kula chakula chenye sumu hiyo.
“Ukiona maji yana zebaki huenda kuna mwamba wenye madini hayo sehemu maji hayo yanakopita. Mkaa wa mawe huambatana na madini yaitwayo sulfide ambayo hubeba zebaki pia,” anasema Dk Mshiu na kuongeza:
“Ipo haja ya kupima maeneo mengine kujua chanzo halisi cha madini hayo,” anasema Dk Mshiu.
Aliyekuwa mkurugenzi wa kinga wa Wizara ya Afya, Dk Ali Mzige anasema“zebaki hupunguza kinga za mwili, nguvu za kiume na mjamzito anaweza kujifungua mtoto aliyeathirika ambaye hatokua vizuri. Hatua zisipochukuliwa kijiji kizima kinaweza kuathirika. Hushambulia mfumo wa kati wa fahamu.”
Muuguzi na mkunga wa Zahanati ya Ndumbi, Rehema Mbunda anasema hakuna bomba la maji kijijini hapo na watu wote wanategemea maji ya ziwani.
Kutokana na ukweli huo, anasema kila mjamzito hulazimika kwenda na maji yake atakayoyatumia kuoga, kufua na usafi mwingine vinginevyo, ndoo moja ya lita 20 huuzwa Sh500.
“Mara chache, tunapozidiwa sana, huwa tunawaomba wajawazito wanaokuja kliniki watusaidie kuchota maji,” anasema Rehema.
Kwa upande wake, mganga mkuu msaidizi wa Zahanati ya Ndumbi, Samson Bukuru anasema wakati anaripoti kituoni hapo mwanzoni mwa mwaka jana alikuta malaria ndio ugonjwa unaoongoza, lakini kwa juhudi zake za kuelimisha jamii sasa hivi maambukizi ya koo ndio yapo juu zaidi.
“Wagonjwa wa neva na misuli, ganzi ya magoti, shingo na mikono pamoja na matatizo ya figo yapo sana. Wagonjwa wa ngozi pia tunawapokea mara kwa mara. Yapo yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyo salama,” anasema Bukuru.
Wakati ripoti ya mwaka 2018 ikiandaliwa, takwimu za zahanati hiyo zinaonyesha malaria na magonjwa ya mfumo wa hewa ndiyo yalikuwa yanaongoza yakifuatiwa na nimonia, athma na magonjwa ya ngozi.
Mengine kwenye orodha hiyo ni minyoo, magonjwa ya zinaa, maambukizi ya macho, fangasi, kuhara na kuharisha.
Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Lituhi, Dk Isaac Kyando anasema tangu alipoanza kufanya kazi hospitalini hapo Agosti 2018, wagonjwa ya ganzi ya miguu, mikono na shingo ni wengi zaidi.
“Huwa nakutana na wenye magonjwa yasiyoambukiza kila wiki. Kuna mafanikio yanaonekana, ila, tunayo changamoto moja kubwa, upatikanaji wa maji,” anasema Dk Kyando.