Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maji yatiririka kwa wakazi 13,279 wa Mbesa

79db85ffb29c8201af4618f2530f83e5 Maji yatiririka kwa wakazi 13,279 wa Mbesa

Wed, 3 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

ZAIDI ya wananchi 13,279 wa vijiji vya Nasomba Kata ya Nalas Mashariki na Mbesa kata ya Mbesa wilayani Tunduru, wameanza kunufaika na miradi mikubwa ya maji iliyogharimu Sh 253,117,473 zilizotolewa na Wizara ya Maji.

Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini na Usafi wa Mazingira (Ruwasa) Wilaya ya Tunduru, Primy Damas alisema miradi hiyo yote imekamilika kwa zaidi ya asilimia 100 na wananchi wameanza kupata huduma ya maji safi na salama kwenye maeneo yao.

Damas alisema mradi wa maji Kijiji cha Nasomba umetekelezwa kwa gharama ya Sh 150,554,761 zilizotolewa na Benki ya Dunia ambapo zaidi ya wakazi 3,500 wamenufaika.

Ulianza kujengwa Mei 2020 na kukamilika Desemba 2020 kwa kuwatumia mafundi wadogo. Alisema, katika mradi huo kazi zilizopangwa kufanyika na zilizofanyika ni kujenga tangi la juu la ujazo wa lita 50,000, nyumba ya mitambo, ununuzi wa mabomba yenye ukubwa tofauti za umbali wa mita 3,200 na viungio vyake.

Damas alisema kazi zingine zilizofanyika ni ununuzi na ufungaji wa nishati na mfumo wa umeme wa jenereta,ununuzi na ufungaji wa pampu kwa ajili ya kisima,uchimbaji mitaro,ulazaji mabomba na ufikiaji mitaro na kujenga vituo vinane vya kuchotea maji.

Aidha, mradi wa maji Mbesa ulitengewa Sh 102,562,712 ambazo zinaendelea kutumika kwa ajili ya kuwaondolea kero ya maji takribani wakazi wapatao 9,779 wa kijiji hicho.

Alisema katika bajeti ya mwaka huu Wizara ya Maji imeipatia Ruwasa wilaya ya Tunduru Sh 2,582,124,451.2 kwa ajili ya kukamilisha na kujenga miradi katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Chanzo: habarileo.co.tz