Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maji yageuka fursa Dar

Maji Dar Balaa Maji yageuka fursa Dar

Mon, 14 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kufa kufaana! Ni msemo unaoonekana kuakisi kinachojiri Dar es Salaam kutokana na uhaba wa maji ulioukumba mkoa huo.

Wakati shida hiyo ikiwa maumivu kwa wakazi wengi wa Dar es Salaam, kwa baadhi ya watu, wakiwamo madereva pikipiki za kubeba abiria (bodaboda), imegeuka fursa.

Kwa wanaonunua maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, sasa wanauziwa na bodaboda kwa galoni la lita 20 kwa wastani wa Sh. 1,000 hadi 2,000, Nipashe ikishuhudia utaratibu huo kwenye maeneo ya Bunju A, Bunju B, Tegeta, Mbezi Beach, Mabwepande na Mbweni.

Nipashe imebaini baadhi ya vijana wanaofanya biashara ya bodaboda sasa wamechana na kusafirisha abiria na kuhamia katika kuuza maji, wakitamba biashara hiyo mpya kwao inawalipa zaidi kulinganishwa na kubeba abiria.

"Kubeba maji kwa sasa ndiyo habari ya mjini, inalipa zaidi kuliko kubeba abiria. Na kwa sisi ambao tunapeleka hesabu kwa mabosi wetu kwa sasa hatuumizi kichwa kabisa," alisema Sudi Mavinzo anayefanya biashara hiyo ya maji katika eneo la Bunju B.

Katika mazungumzo na Nipashe jana, Mavinzo alisema ana wiki tatu tangu aanze biashara hiyo ya kuuza maji, akibainisha kuwa kwa sasa anao uhakika kupata si chini ya Sh. 50,000 kwa siku.

"Na sio kwamba unatafuta wateja, hapana! Ni wengi mpaka unawakataa mwenyewe. Kwa hiyo, inanilazimu niamke alfajiri, ili nipambane nao.

"Na wateja wangu ni wa aina mbili, wa kwanza ni hawa wanaotaka ukachote mwenyewe halafu uwauzie, lakini kuna wengine ambao wanatafuta maji yanakotoka au wanachota kwa kwenye visima madumu mengi halafu unawabebea kuwapelekea nyumbani," alisema.

Dereva bodaboda huyo alibainisha kuwa wateja wanaonunua kwa dumu moja, huwauzia kwa Sh. 700 na wale wa kuwapelekea nyumbani baada ya kuchota wenyewe huwatoza kulingana na umbali wa eneo wanakoishi.

"Kwa mfano, kwa mita 200 kwa madumu sita ninawatoza Sh. 3,000, ikiwa mbali zaidi, ni Sh. 6,000 kwa madumu sita," alifafanua.

Eliya Lucas, mkazi wa Mbweni anayejishughulisha na udereva wa bodaboda, alisema wateja wake wengi ni wanaotoa oda ya kupelekewa maji nyumbani.

"Mwingine anaweza kukuagiza umchotee madumu 30 au 20, na kwa siku ninaweza kupata oda ya watu watano, wanane hadi 10.

"Kwa sababu wengi nimewazoea, ninawatoza dumu kwa Sh. 500 mpaka 600, na kule ninakochota mimi ninalipia Sh. 200 kwa dumu. Kwa hiyo, kinachohitajika ni nguvu yangu inapoishia.

"Kuna wakati ninabeba maji mpaka kiuno kinagoma, ukiinama unapata maumivu makali, kwa sasa nikiona oda inanizidia, ninawaomba wenzangu tunasaidiana, wananipa fedha kidogo kwenye kila dumu halafu wanabaki na chao. Kwa siku mapato yangu sasa hayapungui Sh. 40,000 mpaka 60,000," alisema.

Theophil Thomas, dereva bodaboda eneo la Mbezi Beach, alisema kwa sasa amepunguza idadi ya abiria na nguvu yake amewekeza zaidi katika kuuza maji.

"Huu uhaba wa maji kwa kweli kwa namna moja au nyingine kwetu sisi tumefaidika, hatufurahii kwa sababu imekuwa hivi lakini hatuna namna inabidi tuwasaidie na sisi tupatie japo kipato chetu.

"Mimi sijaacha kabisa kubeba abiria, nina wateja wangu wa kudumu ambao siwezi kuwaacha. Kwa hiyo, ninawabeba kama kawaida," alisema Theophil na kubainisha kuwa dumu moja la maji ananunua kwa Sh. 200 hadi 250 na kuyauza kwa Sh. 700 na kipato chake kwa siku kinaanzia Sh. 30,000 hadi 40,000.

MAUMIVU

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Nipashe mkoani hapo mwishoni mwa wiki, walisema pamoja kutangaziwa kwamba watakuwa wanapata maji kwa mgawo, wengi  hawafikiwi na mgawo huo.

"Mimi ninaishi hapa Bunju A, nina mwezi  sasa huo mgawo wa maji sijawahi kuupata, nina familia kubwa, ninalazimika kutumia fedha nyingi kila siku kununua maji kwa hawa bodaboda wanaouza kwenye madumu," alisema mkazi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Mama Junior.

Mkazi mwingine wa mkoa huo aliyejitambulisha kwa jina moja la Hanifa, alisema anaishi Mbweni Mpiji na hajapata maji ya mgawo tangu ulipotangazwa.

"Nilichobakiza ni kuomba neema ya Mungu tu ashushe mvua, la sivyo sijui itakuwaje. Nina familia ambayo inanilazimu nitumie si chini ya Sh. 15,000 kila siku, maana vyoo vyangu ni vya kutumia maji zaidi na nisipofanya hivyo tutapata maradhi," alisema Hanifa.

Joseph Birundula, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, alidai wana wiki mbili pasi na kupata maji ya bomba, hivyo wamehamia katika matumizi ya maji ya visima ambayo anaona si salama kiafya, akiomba mamlaka kupima maji hayo ili wananchi wasiathirike.

"Sio mimi tu niliyeshtukia hili suala, kuna baadhi ya maeneo wanakouza chakula wanalalamikiwa kwamba wanalisha watu chakula kilichopikwa kwa maji ya chumvi, pia juzi pale ninapofanyia kazi kuna mtu alimuuzia kijana uji wa mchele alipounywa alikuta una chumvi nyingi ilibidi aumwage," alidai Birundula.

Zainabu Rashidi, mkazi wa Tabata, aliomba watumishi wa Mamlaka ya Maji (DAWASA) wanaoratibu utaratibu wa mgawo wa maji, kuhakikisha wanasimamia suala hilo kwa weledi bila upendeleo kwa kuwa mitaa yao yaijaona maji ya mamlaka hiyo kwa wiki mbili sasa.

Issa Mduma, dereva bodaboda anayeuza maji, alisema anatumia muda mwingi kuuza maji kuliko kubeba abiria kwa kuwa anapata fedha nyingi.

"Biashara ya maji imekuwa ikiniingizia fedha zaidi kwa kipindi hiki, muda wote unakuwa unauza maji tofauti na kubeba abiria ambao tulikuwa tunawasubiria kituoni kwa muda, japokuwa wamiliki wa pikipiki wanakuwa hawataki tubebe maji lakini tunapita katika mitaa ambayo sio rahisi kutuona," alisema Mduma.

Hivi karibuni viongozi walibainisha njia mbalimbali za kukabiliana na upungufu wa maji katika Mkoa wa Dar es Salaam ikiwamo kufufua visima.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Dar es Salaam sasa inakabiliwa na upungufu wa maji lita milioni 120 kutokana na uzalishaji wa sasa kuwa lita milioni 400 kwa siku.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live