Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maji toka Ziwa Victoria yalivyoboresha maisha Tabora

D2efe362c011e9ea2ac4b143139caf22.png Maji toka Ziwa Victoria yalivyoboresha maisha Tabora

Mon, 31 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MOJA ya eneo alilogusia Rais John Magufuli wakati akilihutubia kwa mara ya mwisho Bunge la 11 kwamba serikali yake inalishughulikia kwa umakini mkubwa ni uboreshaji wa huduma za majisafi na salama kwa watanzania.

Mwaka 2015 wakati serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani, kiwango cha upatikanaji wa maji kwa maeneo ya vijini kilikuwa asilimia 47 lakini takwimu za mwaka huu zinaonesha kwamba huduma hiyo imepanda hadi kufikia asilimia 70.1.

Aidha kwa upande wa mijini huduma ya upatikanaji wa maji nayo imepanda kutoka asilimia 74 mwaka 2015 hadi asilimia 84 mwaka huu.

Eneo moja ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kuwezesha mafanikio hayo ni mradi wa kusafirisha maji kutoka ziwa Victoria hadi mkoani Tabora ambao unasimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama na Shinyanga (KASHWASA).

Hadi Februali mwaka huu taarifa kutoka Wizara ya Maji kuhusu utekelezaji wa mradi huo katika miji ya Nzega, Tabora, Igunga na Uyui, ilionesha kuwa miji yote hiyo pamoja na vijiji 92 vilivyoko maeneo hayo vilikuwa vimefikiwa na huduma ya maji hayo safi wakati vijiji 10 vikitarajiwa kufikiwa pia.

Hili siyo dogo kwa sababu maeneo hayo kwa kawaida yana hali ya ukame na hivyo kuwa na upungufu wa maji yanayotosheleza wananchi misimu yote. Hata wale waliokuwa wanapata maji ya bomba hawakuweza kuepuka mgao wa maji.

Hali hiyo imekuwa ikiathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya wakazi wa maeneo hayo kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta maji. Raslimali fedha nyingi pia zilikuwa zikitumika kwa ajili ya kununua maji kulinganisha na maeneo mengine yenye uhakika wa maji.

Magonjwa ya kuambukiza hasa yale yanayotokana na matumizi ya maji yasiyosalama yamekuwa pia yakitajwa sana katika maeneo haya.

Hivyo hatua ya upatikanaji wa huduma ya maji ya uhakika ni mwanzo wa mabadiliko chanya katika kuboresha maisha ya wananchi wa maeneo husika.

Ukitembelea mitandao ya kijamii ikiwemo YouTube, kutumia viunganishi hivi: https://www.youtube.com/watch?v=3mbOrDftDwg pamoja na https://www.youtube.com/watch?v=0wG6iVJiIOk unaweza kuwasikia namna wananchi wa miji hii wanavyoishukuru serikali kwa kusikia kilio chao cha muda mrefu cha kumaliza tatizo la uhaba wa maji.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, anasema ujio wa maji umeileta Toronto ya kweli Tabora aliyoihubiri kwa muda mrefu.

Kabla hajastaafu alisema changamoto ya magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyosalama ikiwemo homa ya matumbo na magonjwa ya kuhara imepungua sana mkoani Tabora mara baada ya mradi wa kufikisha maji katika maeneo ambayo hayakuwa na huduma hiyo kukamilika.

Mwanri anawaalika wawekezaji kwenda mkoani Tabora kuwekeza kwani changamoto kubwa za mkoa huo ikiwemo huduma ya maji sasa imetatuliwa na serikali.

“Hakuna mwekezaji anayetamani kwenda kuwekeza katika eneo ambalo lina uhaba wa maji. Toronto ya kweli sasa imefika. Niwaombe Watanzania wote, wakiwemo wakazi wa Mkoa wa Tabora walioko ndani na nje ya nchi waje kuwekeza nyumbani,” anasema Mwanri.

Pili Mweda, mkazi wa Kijiji cha Mwanzugi wilayani Igunga anasema kwa muda mrefu walikuwa wanalazimika kuchangia maji na mifugo wakati huo wakitegemea maji kutoka bwawa la Mwanzugi.

Naye Edina Philipo, Mkazi wa Igunga anasema iliwahi kutokea wakavamiwa na watu ambao walishindwa kuwatambua wakati wakienda kuchota maji nyakati za usiku.

“Mimi mwenyewe niliwahi kukimbizwa usiku wakati nikifuata maji. Bahati nzuri nilikimbia huku nikapiga kelele hadi aliyekuwa akinikimbiza akaniacha. Kwa kweli ujio wa maji haya umepunguza matatizo mengi ya kifamilia huku kwetu,” anasema.

Mathias John, Mkazi wa Ziba, Kitongoji cha Igumila wilayani Nzega anasema kwamba uhaba wa maji ulikuwa umeleta utaratibu mpya wa maisha.

Anafafanua kwamba badala ya utaratibu wa kawaida katika maeneo mengi maji kuchotwa na akina mama, kazi hiyo ilikuwa ikifanywa na akina baba kwa kutumia maguta, mikokoteni au baiskeli.

Akiongelea mabadiliko baada ya mradi mpya kuanza kazi, Elifuraha Mpanda anayeishi Mtaa wa Mwayunge Wilayani Igunga anasema maji yamemfanya aione fursa mpya ya kilimo cha bustani ya mbogamboga na ufyatuaji wa matofali kwa ajili ya biashara.

“Nafurahi sasa nimeiona fursa mpya kupatia upatikanaji wa maji. Nafyatua matofali, nauza, nalima bustani na kuzalisha mbogamboga ambazo zinaniongezea kipato huku wananchi wakunufaika na lishe bora,” anasema.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira wilayani Igunga, Raphael Melumba anasema kabla ya mradi, kuna wakati serikali ilikuwa inalazimika kuingia gharama kubwa kusomba maji kuwapelekea wananchi kwenye maeneo yao.

“Kwa mfano, mwezi wa Oktoba mwaka jana tulilazimika kuingia gharama ya kusomba maji kuwapelekea wananchi kwenye maeneo yao kutokana na ukame uliosababisha kukauka kwa mabwawa yote likiwemo bwawa la Bulenya ambalo wamekuwa wakilitegemea,” anasema Melumba.

Wanachi wengi wanakiri kwamba ujio wa maji unafungua fursa nyingi za kiuchumi mkoani Tabora na kupunguza gharama za maisha kwa familia zao.

Mzee Lumanila Kija wa Kijiji cha Ziba wilayani Nzega anasema gharama za maji zimepungua kutoka kati ya shillingi 500 hadi 1000 kwa ndoo hadi kati ya shilingi 30 na 50 kwa ndoo.

Mzee huyo anasema angekuwa bado ni kijana, angeweza kufanya makubwa kwa sababu alishindwa kufanya mengi wakati wa ujana wake ulioshia kijijini hapo kutokana na sehemu kubwa ya muda wake kuutumia kwa kutafuta maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya familia.

Adamu John wa kijiji hicho cha Ziba anasema ujio wa maji umemfanya aanze biashara ya kuchuuza maji ambapo kwa sasa anawapelekea wananchi majumbani mwao hasa wale ambao hawana nafasi ya kufika kwenye vioski vilivyojengwa na serikali kwa ajili ya kutoa huduma hiyo kwa wananchi wote.

Kazi hiyo anasema imemwezesha kununua baiskeli mpya na sasa ameanza ujenzi wa nyumba ya kudumu.

Maji yameleta pia fursa ya kilimo cha biashara kama anavyosema Saada Juma, mkazi wa Nzega ambaye ameanza pia kulima bustani ya mbogamboga baada ya kuwa na uhakika wa maji.

Agostino Maridadi, mkazi wa Mwanzugi, Igunga, anasema yeye ameanzisha biabiashara ya tofali ambapo anafyatua, kuchoma na kuuza. Hilo anasema limemsaidia kujikwamua kiuchumi na kukidhi mahitaji ya familia.

Tabasamu walizonazo wananchi kufautia upatikani wa maji wa uhakika unaonesha kwamba ndoto ya kumtua mama ndoo inaendelea kutimizwa na serikali ya awamu ya tano, kazi inayoendelea katika maeneo mengine ya nchi.

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni [email protected], 0717697205.

Chanzo: habarileo.co.tz