Majeruhi 40 kati ya 44 wa ajali ya basi la Sheraton iliyosababisha vifo vya watu 10 waliolazwa kwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Geita wameruhusiwa kutoka hospitali baada ya hali zao kuimarika.
Katika ajali hiyo ilitokea eneo la Ibandakona Kata ya Kasamwa wilayani Geita Machi 7,2023, watu 10, akiwemo Mwandishi wa habari wa gazeti la Nipashe, Richard Makore walifariki dunia na wengine 48 kujeruhiwa ambapo wanne kati yao walitibiwa na kuruhusiwa.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Geita, Dk Pasclates Ijumba amesema kufikia mchana wa leo Ijumaa Machi 10, 2023, majeruhi wanne pekee ndio wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo na hali zao zinaendelea vizuri.
Amesema hata wawoto wawili, mmoja mwenye umri wa miezi nane na mwingine mwenye miaka mitatu waliokuwa wanatunzwa hospitalini hapo tayari wamechukuliwa na ndugu baada ya mwili ya mama zao waliofariki kwenye ajali hiyo kutambuliwa.
“Miili ya watu wote 10 waliofariki katika ajali hiyo pia imechukuliwa na ndugu kwa ajili ya mazishi,” amesema Dk Ijumba
Akizungumzia ajali hiyo, Ikorongo Otto, mkazi wa mjini Geita ambaye pia ni Katibu wa chama cha ACT-Wazalendo mkoani humo ameiomba Serikali kupitia mamlaka husika kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa ubora wa vyombo vya usafirishaji ili kudhibiti ajali zinazoweza kuzuilika na kunusuru mali na maisha ya watu.
“Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani iongeze nguvu kwenye ukaguzi na kuzuia magari yote yasiyo na ubora kusafirisha abiria,” ameshauri Otto.