Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majambazi wavamia mabasi na malori, wapora na kutokomea

Kamanda Wa Polisi Mkoa Wa Njombe, Hamis Issah RPC wa Njombe, Kamanda Issah

Fri, 24 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu wanaodhaniwa kuwa ni Majambazi wamevamia magari zaidi ya saba (7) ikiwemo magari ya mizigo pamoja na basi la abiria katika eneo la Nyaliva katikati ya kijiji cha Nyombo na Kidegembye barabara ya Njombe - Lupembe Halmashauri ya Wilaya ya Njombe wakidaiwa kupora fedha na simu za abiria.

Wakizungumza na vyombo vya habari, baadhi ya Mashuhuda wa tukio hilo Mwamini Hongoli ambaye ni Kondakta wa Basi na Bernad Kawogo Dereva wa Basi ambaye amejeruhiwa kwa kupigwa na bapa la panga amesema uvamizi huo ulitokea wakiwa safarini huku Wavamizi wakiwa wameficha nyuso zao kwa kwa mask.

Dereva huyo amenukuliwa akisema; “Nilipofika eneo lile nilikuta magari yamepaki sasa Mimi nikawa napita pembeni, mbele yangu tena nikaona zimepaki gari za mnada niliposimama tu nikapigwa na panga kwenye shavu huku wakiniambia rudi kwenye gari yako wakati huo Kondakta wangu akiwa ameshalazwa chini."

Naye Mwamini Hongoli Kondakta wa gari hilo ameeleza; “Kwa kuwa lengo lao lilikuwa ni pesa waliokuwa Wabishi walipigwa sana mimi niliwapa Tsh. Elfu 13 na kulala kifudifudi kwahiyo baada ya dakika kadhaa tukaona pako kimya ndio tukatoa magogo yaliyokuwa yametegwa ili magari yaweze kupita."

Dr. Ayubu Mtulo ambaye ni Kaimu Mganga Mfawidhi Hospitali ya Mji Njombe amekiri kupokea majeruhi huyo mwenye umri wa miaka 39 ambaye anaendelea na matibabu huku RPC wa Njombe Hamisi Issa akizungumza kwa ufupi kwa njia ya simu na kusema kuwa yupo eneo la tukio wakiendelea na uchunguzi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live