Arusha. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassimu Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya kumbukumbu ya kugunduliwa fuvu la Zinjanthropus Julai 22 mwaka 2019, katika makumbusho ya Olduvai, ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo, Profesa Audax Mabula akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Julai 15,2019 amesema Majaliwa anatarajiwa pia kuzindua makumbusho ya watafiti waliogundua fuvu hilo, Julai 17 mwaka 1959, Dk Louis Leakey na mkewe Dk Mary Leakey.
Amesema makumbusho ya watafiti hayo, ambayo yametunzwa na Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, kuna vifaa mbalimbali walivyokuwa wakitumia, nyumba waliokuwa wanalala, gari waliyokuwa wanatumia.
"Haya ni makumbusho ya kihistoria duniani katika masuala ya utafiti wa kujua chimbuko la binaadamu na hadi sasa eneo la Olduvai ndilo linatambulika ni moja ya maeneo duniani ambayo watu wa kale na wanyama wa aina mbalimbali waliishi," amesema
Profesa Mabula amesema kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni tujivunie urithi na chimbuko letu, ambapo watafiti kutoka maeneo mbalimbali duniani, watalii wa ndani na nje watapata fursa ya kutembelea makumbusho na maonesho ya urithi wa tamaduni.
Meneja Idara ya Urithi wa Utamaduni wa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, Joshua Mwaikunda amesema wameandaa ofa ya kutembelea makumbusho ya Olduvai katika maadhimisho hayo ambayo yataanza Jumatano ya Julai 17,2019 yakiambatana na warsha ya watafiti kutoka maeneo mbali mbali duniani.
Pia Soma
- Zuma adai tuhuma za rushwa dhidi yake zilipikwa na shirika la upelelezi la kigeni
- Polisi waendelea kumng’ang’ania Halima Mdee
- VIDEO: Magufuli azindua nyumba za askari, atoa agizo kwa IGP Sirro
"Kunakuwa na maonesho ya maeneo yote ya kale, ikiwepo Kondoa Irangi, makumbusho ya taifa na maeneo mbalimbali nchini yenye urithi wa utamaduni," amesema
Meneja uhusiano wa NCAA, Joyce Mgaya ametoa wito kwa Watanzania na wageni kutembelea makumbusho ya Olduvai kujionea historia ya binaadamu ambayo haipatikani sehemu yoyote duniani.
"Hii ni fursa ya kipekee kwa watanzania ma watafiti duniani kukutana Olduvai kujifunza mambo kale na kujionea urithi wa utamaduni uliopo nchini," amesema.