Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa awataka wakurugenzi wa halmashauri kuchapa kazi

Fri, 4 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Songea. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini Tanzania wafuatilie utendaji kazi wa watumishi kwenye maeneo yao kubaini kama wanakwenda kwa wananchi na kuwahudumia ipasavyo.

“Serikali inahitaji kuona watumishi wa umma wanakwenda kwa wananchi  kusikiliza kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kushirikiana nao kuzipatia ufumbuzi,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo jana Alhamisi, Januari 3, 2019 wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Lugagala, wilayani Songea akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma.

“Rais wetu John Magufuli ni muumini wa maadili na mchapakazi, ndio maana amesisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kwenda kuwahudumia wananchi katika maeneo yao, baadhi yao hawana uwezo wa kufikia maeneo ya kutolea huduma,” amesema.

Amebainisha kuwa ni vyema watumishi wa umma kuhakikisha wanapanga muda wa siku tatu kwa wiki kutoka ofisini kwenda kuwahudumia wananchi hususani waishio maeneo ya pembezoni.

Alitumia fursa ya mkutano huo kuwataka wananchi waendelee kuiamini Serikali yao pamoja na watendaji wake waliopo kwenye maeneo mbalimbali.

Amesema Serikali haina msamaha na watumishi wazembe, hivyo wananchi waendelee kuwa watulivu na imani kwani watahudumiwa na ahadi zote zilizotolewa na Rais katika maeneo yao zitatekelezwa.

Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Songea asimamie zoezi la kuwaondoa wananchi wote wanaoishi na kufanya shughuli za katika maeneo ya vyanzo vya maji kwa sababu watasababisha vyanzo hivyo vikauke.

Awali, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Luyehela kwenye kijiji cha Muungano Zomba, kuzindua kituo cha kuchotea maji cha kijiji cha Lugagala na kukagua mradi wa ujenzi ya zahanati wa kijiji hicho.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, ,Jenister Mhagama na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga.



Chanzo: mwananchi.co.tz