Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka watoto wa kike wasikubali kudanganywa na wanaume na badala yake wakazanie masomo hadi wahitimu elimu ya juu.
Majaliwa ametoa wito huo kwa nyakati mwishoni mwa wiki tofauti wakati akizungumza na wakazi wa wilaya za Same na Mwanga akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo mkoani Kilimanjaro.
“Wasichana wote mliopo hapa, mwanaume yeyote akikufuatafuata mwambie usinisumbue; mwambie niache nisome. Kamwe msikubali kudanganyika, someni hadi mmalize Chuo Kikuu,” alisema Majaliwa
Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Julai 22, 2019 na Ofisi ya Waziri Mkuu imesema Majaliwa ambaye alikuwa na ziara ya siku nne mkoani humo, amewaonya vijana na wazee ambao wana tabia ya kuweka mahusiano ya kimapenzi na watoto wa kike kwamba waache mara moja la sivyo wataishia jela.
“Wanaume msisahau kwamba mtoto wa mwenzio ni wako. Nataka niwakumbushe kuwa ukimuona mtoto wa kike, muache. Huyo ni moto wa kuotea mbali. Ukimchumbia, ukimuoa, au kumpa mimba mtoto wa kike, ujue kuwa miaka 30 jela ni yako.”
“Serikali ya awamu ya tano, imeamua kuwekeza kwa mtoto wa kike, kwa hiyo tunataka watoto wa kike wakianza shule ya awali, wasome shule ya msingi, waende sekondari hadi wamalize Chuo Kikuu,” alisisitiza.