Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa atua Ruangwa, atoa maagizo kwa ofisi elimu

68560 Pm+pic

Sun, 28 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim wa Tanzania, Majaliwa amemwagiza Ofisa Elimu wa Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi anayeshughulikia elimu ya msingi, Selemani Mrope atafute walimu wawili kutoka wilayani humo na kuwahamishia kata ya Nanganga ili kupunguza changamoto  ya upungufu wa walimu katika kata hiyo.

Waziri Mkuu ambaye amewasili Lindi leo Jumamosi Julai 27, 2019 kwa mapumziko mafupi, ametoa agizo hilo akiwa katika kata ya  Nanganga baada ya kupokea taarifa ya shule ya msingi Nanganga ambayo ilionyesha shule hiyo yenye wanafunzi 237 ina walimu sita tu.

"Lazima kuna walimu wamejazana pale Ruangwa mjini, leo tukitoka hapa nenda kaandike barua za uhamisho. Kesho Jumapili, wahusika wapewe barua zao na Jumatatu waje kuripoti hapa Nanganga," amesema Waziri Mkuu na kuamsha shangwe miongoni mwa wakazi wa Nanganga. 

“Shule hii ina madarasa nane likiwemo darasa la awali, masomo yanayofundishwa ni tisa, mkibaki na walimu hawa sita, mzigo unakuwa mkubwa kwa walimu hawa waliopo. Ofisa elimu tafuta wawili walimu waje hapa Jumatatu na mkurugenzi wa halmashauri atakupa gari ya kuwahamishia hapa,” amesema. 

Waziri Mkuu ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa, amewataka wakazi wa kata hiyo wafikirie kuanza ujenzi wa shule ya sekondari yao ya kata ili kuwapunguzia safari wanafunzi wa kijiji hicho ambao kwa sasa wanalazimika kwenda kusoma Nangumbu, iliyoko umbali wa kilomita 10.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, Serikali imetoa Sh60 milioni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne ambayo yakikamilika walimu watapata ofisi pia.

Pia Soma

Amesisitiza kwamba fedha hizo zitumike kujenga madarasa manne ambapo walimu pia watapata ofisi moja. 

Akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Amiri Musa Kambona amesema  madarasa mawili na ofisi moja ya walimu vilibomoka mwaka 2014 kutokana na mvua na upepo mkali na kusababisha upungufu wa madarasa na ofisi.

Akielezea changamoto nyingine za  shule hiyo, Mwalimu Kambona alisema shule ina upungufu wa nyumba moja ya walimu, darasa moja, matundu mawili ya vyoo vya walimu, ofisi moja ya walimu na kukosekana kwa chanzo cha maji safi na salama kwa matumizi ya wanafunzi na walimu. 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz