Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa ataka benki zilizopo mikoa inayolima pamba kufunguliwa kesho

69724 Pic+majaliwa

Sun, 4 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania,  Kassim Majaliwa amezitaka benki zilizoko kwenye Mikoa inayolima pamba kuhakikisha kesho Jumapili Agosti 4, 2019 zinatoa  huduma kwa wanunuzi wa pamba.

Amesema lengo ni wakulima kukamilisha taratibu za mikopo na kuanza kulipwa Jumatatu Agosti 5, 2019.

Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Agosti 3, 2019 na ofisi ya Waziri Mkuu imemnukuu Majaliwa akisema benki hizo zikifunguliwa itasaidia wanunuzi kukamilisha taratibu mbalimbali kabla ya kuanza kulipa wakulima hao Jumatatu.

Majaliwa ametoa wito huo wakati akizungumza na wakuu wa Mikoa nane inayolima pamba ya Mara, Mwanza, Simiyu, Geita, Kagera, Shinyanga, Singida na Tabora pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB.

“Kesho benki zinazotoa  huduma Jumapili ni vema zifanye kazi  ili wanunuzi wa pamba waje wakamilishe taratibu zote za makaratasi na Jumatatu wapate hela ya kuanzia kazi. Hata mkifunga saa 6 mchana, wao wabakie hadi saa 10 jioni ili mradi wakamilishe taratibu zote,” amesema.

Waziri Mkuu amesema kikao kilichofanyika jana kati ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wanunuzi wa pamba na wamiliki wa mabenki walikubaliana kuanza kutoa mikopo kwa wanunuzi ili waanze kununua pamba Agosti 4, 2019.

Pia Soma

Mwenyekiti wa wamiliki wa Mabenki, Abdulmajjid Nsekela, aliwahakikishia wakuu wa mikoa yote na wanunuzi waliokuwa wakishiriki mkutano huo, kuwa fedha itapatikana kuanzia Jumatatu.

Mwenyekiti wa wanunuzi wa Pamba, Christopher Gachuma amesema wanunuzi wako tayari kununua pamba ili itoke mikononi mwa wakulima.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amewataka wanunuzi wa pamba katika Wilaya za Meatu, Igunga na Singida kupeleka katika viwanda maalum za kuchambua mbegu na siyo vya kusindika mafuta.

Mbali na tahadhali hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Selemani Jafo ameiomba BoT kusimamia kwa karibu makubaliano ya kikao hicho ili kufanikisha utekelezaji  kwa haraka zaidi.

Chanzo: mwananchi.co.tz