Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepokea mapendekezo kutoka kwa wananchi wa tarafa za Loliondo, Ngorongoro na Sale kuhusu namna bora ya kulinda uhifadhi wa maeneo hayo.
Wawakilishi wa wakazi wa wilaya hiyo wakiwemo Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Shangai, malaigwanani, madiwani, wenyeviti wa vijiji, wawakilishi wa wanawake na vijana waliwasilisha maoni hayo ofisini kwa Waziri Mkuu, Mlimwa, Dodoma.
Baada ya kupokea mapendekezo hayo, Majaliwa aliwasisitiza wananchi hao waendelee kuiamini serikali kwa kuwa haiwezi kuwa na mipango mibovu kwa wananchi wake.
"Msisikilize maneno maneno ya watu wa pembeni," alisema.
Akizungumzia kuhusu eneo la Msomera lililoko wilayani Handeni, Tanga yanapoandaliwa makazi kwa ajili ya kuwahamishia wakazi wa Ngorongoro waliokubali kuhama kwa hiari, Majaliwa alisema ujenzi wa nyumba za makazi 103 upo mbioni kukamilika na pia Serikali imepanga kuongeza nyumba nyingine, lengo likiwa ni kufikia nyumba 500 kwa ajili ya wakazi hao.
Kadhalika alisema serikali inaendelea kuimarisha sekta ya mifugo ili kuhakikisha wafugaji wote nchini wanapata tija kupitia shughuli hiyo.