Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametumia dakika moja kuwaombea dua majeruhi na watu waliopoteza maisha yao kwenye ajali ya moto iliyotokea leo asubuhi katika eneo la Msamvu- Mkoani Morogoro.
Ajali hiyo iliyotokana na lori la mafuta kulipuka leo Jumamosi Agosti 10,2019 na kuwaunguza baadhi ya watu waliokuwa wakichota mafuta ambapo imesababisha vifo 62 na zaidi ya 70 kujeruhi.
Akitoa salamu za pole kabla ya kuanza hotuba ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Shirikisho la Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (Tahliso) unaofanyika katika ukumbi wa Nkuruma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) leo Jumamosi, Majaliwa amesema ajali hiyo inasikitisha.
"Mpaka sasa kuna majeruhi zaidi ya 63 hali zao sio nzuri sana, tunawaombea kwa Mungu ili wapone haraka. Ajali hii imetokana na lori na ndugu zetu hawa walienda kujipatia mafuta," amesema Majaliwa.
Akizungumzia mkutano huo, Majaliwa amesema amani na utulivu vilivyopo kwenye vyuo vya elimu ya juu nchini vinaonyesha kuna watu wanatekeleza wajibu wake ipasavyo.
Amempongeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kwa kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi wa elimu ya juu.
Habari zinazohusiana na hii
- Miili ya watu 60 ajali ya lori la mafuta Morogoro imehifadhiwa mochwari, 70 wajeruhiwa
- Vyama vya siasa Tanzania vyatoa rambirambi ajali ya lori Morogoro
- Alichokisema Rais Magufuli ajali ya lori la mafuta Morogoro
- VIDEO: Watu zaidi ya 57 wafariki dunia baada ya lori la mafuta kulipuka Morogoro
Awali, Rais wa Tahliso, Peter Niboye amesema mkutano huo wa mwaka unawakutanisha wajumbe kutoka vyuo vikuu vyote wanachama.
Amesema kabla ya mkutano huo walifanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya awamu ya tano ikiwamo ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge.
Kwa upande wake, Waziri Ndalichako amesema hali ndani ya vyuo vikuu ipo shwari kutokana na jitihada wanazofanya katika kutatua changamoto za wanafunzi.
Amesema katika musimu wa masomo uliopita fedha za mikopo zilifikishwa vyuoni wiki sita kabla havijafunguliwa.