Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa amuagiza Profesa Mbarawa kukagua miradi ya maji Kyerwa

21305 Pm+pic TanzaniaWeb

Tue, 9 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bukoba. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wa amemuagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa kwenda wilayani Kyerwa mkoani Kagera kukagua maendeleo ya miradi ya maji na endapo atabaini ubadhirifu achukue hatua kwa watakaohusika.

 

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Oktoba 7, 2018 baada ya kukagua kiwanda cha kukoboa kahawa cha Nkwenda wilayani Kyerwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Kagera.

 

“Waziri wa Maji na Umwagiliaji atakuja hapa kukagua miradi yote ya maji inayotekelezwa katika wilaya hii na atakapobaini ubadhirifu achukue hatua,” amesema Majaliwa ambaye katika ziara hiyo ameambatana na mkewe Mary.

 

Majaliwa ametoa kauli hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa viongozi na wananchi wa wilaya hiyo baada ya kutoridhishwa na ujenzi wa miradi ya maji.

 

Amesema Serikali ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo wilaya ya Kyerwa ili kuwawezesha wananchi hasa wanawake kushiriki shughuli za maendeleo badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji.

 

Amebainisha kupitia kampeni ya Rais John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, watahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

 

Huku akiwataka wananchi nao kutunza vyanzo vya maji amesema nia ya Serikali ni kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma zote muhimu.

 

Pia, amewaagiza viongozi wa mkoa wa Kagera kuwahamasisha wananchi wake kujiunga na Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF), ambao utawapa fursa ya kupatiwa huduma za matibabu wao na familia zao kwa mwaka mzima bure.

 

Awali, Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate pamoja na mbunge wa viti maalumu mkoa wa Kagera, Oliver Semnguruka walimuomba Waziri Mkuu awasaidie katika uboreshwaji wa huduma za maji na afya.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz