Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa aingilia kati mgogoro wa madiwani, watumishi Ileje

Majaliwa Awapa Maagizo Ma RC Kilimo Cha Michikichi Majaliwa aingilia kati mgogoro wa madiwani, watumishi Ileje

Fri, 24 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, mkoani Songwe kuacha malumbano na badala yake wafanye kazi kwa pamoja.

“Tumeleta Sh2 bilioni za ujenzi wa jengo la halmashauri tangu mwaka jana, lakini ninyi bado mnabishana mjenge wapi. Au mnataka nizirudishe hizo fedha?” amehoji na kujibiwa hapana.

“Tumeleta fedha mjenge jengo jipya, lakini ninyi mnataka mbomoe lililopo ili mjenge jingine wakati hapo hakuna eneo la kutosha kupanua mji wenu. Serikali imegoma msibomoe hayo majengo na badala yake mnatakiwa mwende kujenga eneo la Nyumba 10,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana Alhamisi, Novemba 23, 2023 alipozungumza na watumishi, wakuu wa idara, viongozi na wakuu wa taasisi walioko wilayani Ileje kwenye kikao cha watumishi kilichofanyika katika ukumbi wa RM, Ileje, mkoani Songwe.

Amesema madiwani wana nguvu zote kwenye halmashauri, lakini ni lazima wasikilize ushauri unaotolewa na watalamu. Baraza la Madiwani lilikuwa linalumbana na watumishi juu ya kujenga ofisi za halmashauri hiyo eneo la Itumba (walipo sasa) ambalo ni dogo na wakatoa wazo la kutaka kubomoa majengo yaliyopo ili wajenge mapya.

Maeneo yaliyokuwa yanasababisha mvutano ni Ipapa ambalo lilipendekezwa na watumishi kwa vile ni kubwa na litaweka majengo mengi, ilhali madiwani walitaka lijengwe eneo la Nyumba 10 kwani, tayari palishajengwa ukumbi wa halmashauri.

Pia Waziri Mkuu amewataka watumishi hao wabainishe vyanzo vingine vya mapato, ili kupanua wigo wa ukusanyaji mapato wilayani humo na kwamba Sh1.9 bilioni wanazokusanya kwa mwaka, hazitoshelezi mahitaji.

“Watumishi wa halmashauri kila mmoja ashiriki kubainisha vyanzo vingine vya mapato kwenye eneo lake la kazi. Na heshima ya diwani ni kuona kata yake inachangia mapato kwenye Halmashauri yake,” amesema.

Mapema, Waziri Mkuu alikwenda kukagua hatua iliyofikiwa kwenye ukamilishaji wa miundombinu ya hospitali ya wilaya ya Ileje na baadaye kuzungumza na wananchi kwenye stendi ya Itumba, wilayani humo.

Akitoa ufafanuzi wa hoja zilizotolewa na wabunge wa mkoa huo, Waziri Mkuu amewaeleza wananchi kwamba jukumu la ujenzi wa uzio kwenye hospitali ya wilaya ni la halmashauri kwani, wanapaswa kuonyesha fedha ilyokusanywa imechangia kitu gani kwenye wilaya hiyo.

“Nimeenda kukagua wodi ya wanawake na pia wodi ya wanaume. Wodi hizi ziko umbali wa mita 10 kutoka kwenye makazi ya watu. Tengenezeni nguzo, tafuteni wavu mpige fence ili kulinda eneo la hospitali,” amesema.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake wilayani Mbozi ambako atakagua ujenzi wa barabara ya Ruanda -Nyimbili – Izyila- Itumba yenye urefu wa Kilomita 76.69 kwa kiwango cha lami, atakagua mradi wa usambazaji wa umeme REA III – II katika kijiji cha Ivugula na kuwasha umeme.

Pia, ataweka jiwe la msingi kwenye ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Songwe.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live