Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa aagiza mweka hazina Wilaya ya Mkinga achunguzwe

97681 Pic+majaliwa Majaliwa aagiza mweka hazina Wilaya ya Mkinga achunguzwe

Mon, 2 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanga. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza katibu tawala wa Mkoa wa Tanga, Judica Omari kuchunguza utendaji kazi wa mweka hazina wa Halmashauri ya wilaya ya Mkinga, Juan Mening.

Amesema hajaridhishwa na utendaji wake kwa kuwa ameshindwa kusimamia ukusanyaji wa mapato na hata hicho kidogo kinachokusanywa hakifikishwi Serikali.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Jumatatu Machi 2, 2020 wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mkinga pamoja na wananchi baada ya kufungua jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga akiwa katika ziara  ya kikazi mkoani Tanga.

Amesema Serikali inataka kila mtumishi wa umma nchini awajibike kwa kufanya kazi kwa bidii na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haitowavumilia watumishi ambao ni wezi, wabadhirifu, wavivu  na haitosita kuwachukulia hatua.

“Watumishi fanyeni kazi kwa bidii na msitarajie kuundiwa tume pale mnapofanya vibaya, ukiharibu kazi tunakushughulikia hapo  na huu ndio msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli,” amesema.

Waziri Mkuu aliwaeleza watumishi hao kuwa wanatakiwa wafanye kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni za utumishi wa umma na pia watambue dhamana kubwa waliyonayo, ambayo ni kuwahudumia wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Pia Soma

Advertisement
Majaliwa amewataka Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga kuhakikisha wanakuwa wakali katika usimamizi wa makusanyo ya mapato pamoja na matumizi yake.

Wakati huo huo, Majaliwa ametoa siku 18 kuanzia leo kwa watumishi wa halmashauri hiyo wanaoishi jijini Tanga wawe wamehamia katika kituo chao cha kazi na watakaoshindwa wabaki huko waliko.

Amesema Serikali inataka watumishi wa umma wawajibike na waishi katika vituo vyao vya kazi.

“Nawataka watumishi wote wa wilaya hii wanaoishi jijini Tanga wawe wamehamia hapa ifikapo Machi 20 mwaka huu na wasiohamia waendelee kubaki hukohuko,” amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz