Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa leo Jumamosi Septemba 14, 2019 amezindua mafunzo stadi za kazi kwa vijana na kuagiza halmashauri nchini kutenga fedha kwa ajili ya mikopo ya vijana.
Akizungumza katika viwanja vya Don Bosco Mipango jijini Dodoma, Majaliwa amewataka vijana 5,875 wanaomaliza mafunzo ya uanangenzi kutumia mikopo hiyo kujiajiri.
Amesema mbali na mikopo hiyo, Serikali imeziagiza benki kutoa mikopo kwa vijana ili waweze kujiajiri watakapomaliza mafunzo hayo.
"Mtakapomaliza mafunzo nendeni kwa katibu tawala ili wawaingize kwenye orodha ya mafundi stadi na wapeleke kwenye mikoa," amesema Majaliwa.
Amewaagiza wakuu wa Mikoa katika makongamano ya wafanyabiashara kuwatangazia wawekezaji kuwa wana vijana wenye ujuzi ili kusiwe na ulazima wa kuwatoa wafanyakazi katika maeneo mengine.