Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali inania ya dhati ya kufufua viwanda nchini baada ya viwanda vingi kufa na vingine kusuasua ambapo imebaini kuwa ubanguaji huo una manufaa makubwa kwa nchi.
Ubanguaji wa korosho umesimama kwa miaka mingi nchini ambapo vilikuwepo viwanda katika mikoa inayolima korosho ambayo ni Mtwara, Lindi, Ruvuma na Pwani.
Akizungumza katika alipotembelea kiwanda cha ubanguaji wa korosho cha Organic Growth Limited kilichopo Tandahimba katika mwendelezo wa ziara yake mkoani Mtwara leo Agosti 13, 2023 amesema wanunuzi wa korosho ghafi wanapunguza ajira nchini hivyo ubanguaji ukiongezeka utaleta manufaa makubwa nchini.
“Unajua viwanda vyetu vya ubanguaji wa korosho vilikufa vikawa havifanyi kazi bila sababu sasa tumeshtuka tunataka kurudisha viwanda vya ubanguaji ambapo awali vilikuwa katika maeneo ya Lindi, Kibaha, Newala, Mtwara mjini, Masasi na Mtama,” amesema.
“Hawa wanunuzi wa korosho wanapunguza ajira nchini hata viwanda vyote vilisimama vikawa vinasuasua. Anayetaka aje anunue mbegu ya korosho tukiwa tumefunga kwa kilo moja moja ama nusu kilo,” amesema.
“Kibaya zaidi sisi hatuli korosho mpaka kampeni yaani bila kampeni hatuli na sijawahi kusikia na sijui kama kati yenu ameshawahi kumtuma mtoto kununua korosho kwaajili ya kula majumbani hata madukani hazipo mpaka bodi ya korosho iseme ndio tule korosho ina faida kubwa mwilini ukila unakuwa na afya zinaua wadudu na magonjwa mengine,” amesema.
“Unajua hadi ganda la korosho nalo linahitajika kwenye uwekezaji hii ni fursa kubwa kwetu yanakamuliwa na kupata mafuta hapa hapa nchini ni jambo jema,” amesema.
“Huyu mwekezaji ndio kwanza ameweka fedha anaanza kuwekeza, msitamani kuondoka na korosho hapa kiwandani mkichukua korosho kilo moja na wote mkaondoka nazo mtaua kiwanda nataka kiwanda kifanye kazi kwa muda mrefu ili na sisi tupate faida kama nchi,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Mkurugenzi wa Kiwanda cha Ubanguaji cha Organic Growth Limited, Abida Azizi amesema kuwa uwepo wa kiwanda hiki unaenda kupunguza tatizo la ajira kwa Watanzania.
“Ili kuinua hali ya uchumi kwa wilaya na mkoa kwa ujumla kukamilika kutaleta chachu na hamasa ya uwekezaji nchini ambapo itaaongeza idadi ya viwanda nchini,” amesema Azizi.