Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa: Michango ya rambirambi Mv Nyerere ni ya wafiwa

19040 Pic+pesa TanzaniaWeb

Mon, 24 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema fedha za rambirambi zinazochangwa na Watanzania kutokana na ajali ya Kivuko cha MV Nyerere zitawafikia moja kwa moja wafiwa kupitia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Septemba 24, 2018 wakati akizungumza na wananchi wa Ukara, wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.

Amesema kiasi cha Sh310 milioni alichoambiwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe kimechangwa hadi leo asubuhi hakitatumika nje ya shughuli hiyo kama ilivyokuwa wasiwasi wa Watanzania wengi.

“Wafiwa wote, wataitwa tena na mkuu wa mkoa na kugawiwa fedha hizo ili kuhakikisha kila mmoja anapata pole kutoka kwa Watanzania wenzake na nyingine kidogo ndiyo zitakazotumika katika kujenga mnara na wigo katika makaburi yetu,” amesema Majaliwa na kuongeza: “Msiwasikilize wapotoshaji bali muamini kuwa Serikali ipo nanyi katika kipindi hiki kigumu na inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua,” ameongeza.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa ufafanuzi huo wakati kukiwa na sintofahamu iliyoibuka mara baada ya Serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, kazi, ajira na wenye ulemavu), Jenista Mhagama kutangaza akaunti ya kuchangia.

Akaunti hiyo maalumu imepewa jina la ‘Maafa Mv Nyerere’ namba 31110057246 iliyopo katika tawi la NMB Kenyatta jijini Mwanza

Wananchi walitoa maoni hayo kwa nyakati tofauti kupitia, mitandao ya kijamii ya Mwananchi ya’ Instagram na’ Tweeter’ baada ya  kuweka habari inayohusu Serikali kufungua akaunti hiyo kwa ajili ya kukusanya na kuchangisha fedha zitakazowafikia walengwa wa Mv Nyerere.

Yafuatayo ni baadhi ya  maoni  hayo kwa uchache yaliyotolewa na  wananchi hao kupitia mitandao ya kijamii ya Mwananchi baada ya kuwekwa kwa taarifa hiyo.

Officialafredi alisema bado ya Kagera na Luck Vicent Arusha hayajasahau, labda kama ni akaunti hiyo itakuwa ya hao ndugu moja kwa moja.

Kwa upande wake,  Ruvuma alisema “Hatuchangi tutawapa wenyewe,  Serikali hatuiamini, Kagera mlisema hivyo hivyo, sasa hivi mnataka tukichanga mseme mnanunua kivuko kipya? Hapana hatujasahau toeni namba za waathirika tuwatumie wenyewe si nyinyi,”alisema

Naye Nehemiasimangwa alisema yeye atakwenda mwenyewe akiwa amebeba kilo 20 za mahindi na fedha Sh 1,000 na hataki mtu wa kumuelekeza njia.

Geraldwambura aliungana na Nehemiasimangwa kwa kusema “Bora nisafiri mwenyewe hadi Ukerewe nikawatafute waathirika na niwakabidhi mkononi, ila hiyo sound yenu mhh… hatumpati this time.

Naye Barakabaraka alidai kuwa yeye alichangia Sh500,000 kwenye tetemeko la Kagera lakini  walichofanyiwa wahanga ….Hatoi , labda kuwepo na utaratibu mwingine wa kuchangia moja kwa moja wahusika.

Cellestinakiria alisema kwa ufupi ,“Tumeni namba za waathirika tuwachangie lakini nyie hapana… huku  Mwasyove_tito akitaka pia ziwekwe namba za simu au akaunti ya wafiwa. …

Lakini Davdmwaipopo30 alikuwa na mawazo tofauti akitaka Serikali ipunguze fedha kwenye bajeti ya uchaguzi wa marudio ili ziende kuwafariji wafiwa wa Mv Nyerere.

Kwa upande wa akaunti ya Tweeter @frank_willium alipendekeza fedha hizo zielekezwe kwa waathirika na si kupitia katika akaunti hiyo ya Serikali ili kuondoa sintofahamu kama zilizotokea kwenye tetemeko la Kagera na Luck Vicent.

Kwa upande wake, Augustine@mume_mvumilivu15h15hours alisema “Unaingiwa na utu wa kuchangia lakini nikikumbuka tetemeko la Bukoba naishiwa pozi la kuchangia,”alisema.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz