Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maisha ya gheto kwa watoto wa kike balaa

42564 PIC+GETTO Maisha ya gheto kwa watoto wa kike balaa

Tue, 19 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kati ya simulizi zilizogusa hisia za watu wengi waliohudhuria kampeni ya kutokomeza mimba za utotoni katika wilaya ya Kibiti mkoani Pwani ni maisha ya gheto kwa wanafunzi wa kike.

Wakati Serikali na asasi za kiraia wakipambana kumaliza tatizo la mimba shuleni, bado yapo mazingira hatarishi yanayochangia wasichana kubeba ujauzito, maisha ya gheto yakitajwa kuwa miongoni mwa sababu.

Wanafunzi hao walitoa simulizi hiyo baada ya shirika linalojihusisha na masuala ya kijamii na kisaikolojia kwa watoto (Reppsi) kufanya kampeni ya kutokomeza tatizo hilo katika vijiji vya wilaya za Mkuranga na Kibiti.

Kufanikisha kampeni hiyo, Reppsi ilishirikiana na shirika la Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam linalojihusisha na masuala ya Ukimwi (Pasada).

Mwandishi wa Mwananchi aliyetembelea maeneo ya Kibiti, alishuhudia baadhi ya magheto yakiwa karibu na stendi ya mabasi na vituo vya boda boda yaliyojazana wapigadebe, makondakta na madereva.

Mwanafunzi wa shule ya sekondari Nyamisati, Salma Juma (sio jina lake halisi) anasema kuishi gheto ni balaa kwa kuwa changamoto wanazokutana nazo ni nyingi na kubwa ikiwamo ‘mishale’ kutoka kwa wanaume.

Anasema kwa kuwa wasichana wengi waliopanga wanatokea vijiji vya mbali, mara kadhaa hujikuta wakiishiwa chakula na fedha za matumizi ya kununulia mahitaji muhimu.

“Majaribu huwa magumu msichana anapoishiwa mahitaji muhimu kama chakula. Binafsi huwa naenda kukopa dukani kwa sababu naishiwa mara nyingi. Kuna siku inabidi nijikaze na njaa,” anasema Salma.

“Lakini hali kama hii wengine wanashindwa kuivumilia, fikiria umeenda kukopa hela (fedha) umenyimwa utafanyaje? Wengine ndiyo hapo wanajikuta wamekubali kuingia kwenye mahusiano ya kipenzi.”

Anasema vyumba walivyopanga ni kati ya Sh10,000 na Sh30,000 hivyo, baadhi ya wanaume huwapa ahadi ya kuwalipia kodi kama njia ya kuwanasa.

“Sijawahi ruhusu mtu aje chumbani kwangu kuniharibia maisha na wengi wanaonifuatafuata huwa wananivizia huko nje ninapotoka au kwenda shuleni, wanajua sina wazazi wala walezi hivyo, wanaweza kufanya usumbufu wawezavyo,” anasema mwanafunzi huyo.

Mwanafunzi mwingine, Juliana John (si jina lake halisi) anasema tangu alipoanza kidato cha kwanza miaka mitatu iliyopita alikuwa akiishi gheto.

Anasema japo yupo kidato cha nne ila wapo wenzake walioacha shule kwa mimba huku maisha ya gheto yakitajwa kuwa kishawishi cha kujiingiza kwenye mapenzi wakiwa na umri mdogo.

“Wapo wakware wengi wananifuatafuata ila siwezi kukubali huwa nawaambia wazi nipo hapa kusoma sijafuata mapenzi,” anasema Juliana.

Anasema kati ya makundi yanayowasumbua zaidi ni madereva bodaboda ambao baadhi yao hutumia kipato walichonacho kama mtego wa kuwanasa wasichana walioishiwa pesa za matumizi na chakula.

“Tukiishi shuleni maisha yetu yatakuwa salama na hata yule anayetaka kuwa kama Samia Suluhu (Makamu wa Rais) atafikia ndoto yake,” anasema.

Mkurugenzi Mkazi wa Reppsi, Edwick Mapalala anasema ni hatari kwa mwanafunzi wa kike aliye katika (umri wa kukua/ujana) adolescences age kuishi gheto huku akiwa hana uhakika wa chakula wala pesa kwa ajili ya mahitaji mengine.

“Jambo hili linahitaji mjadala zaidi, tunatakiwa kuunganisha nguvu kuona watoto hawa tunaopigania wasibebe mimba wanaishi maisha salama yasiyo na vishawishi vitakavyowachochea waingie huko,” anasema.

Anasema maisha ya gheto kwa wasichana yanaweza kupunguza jitihada za kufikia Tanzania ya viwanda kwa sababu ya changamoto wanazokutana nazo. “Niwasihi watoto wa kike wasikubali kudanganyika, wasikubali hata kidogo hata kama hali ni ngumu. Mambo yakiwa magumu zaidi waende kusema kwa viongozi na hao wanaume wanaowafuatafuata wakisemewa hawataendelea.”

Awali, Mratibu wa Elimu Kata ya Salale, Erasmus Assenga alisema Serikali imeshakamilisha ujenzi wa mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike lakini wameshindwa kuwahamishia huko kwa ukosefu wa vitanda na chakula.

Anasema mwaka huu pekee, tayari wanafunzi wawili wameacha shule kwa mimba jambo ambalo ni hatari.

“Jiografia ya kata hii, vijiji vingi vipo kisiwani ndio maana watoto inabidi wapangiwe vyumba,” anasema Assenga.

Anasema tatizo la mimba shuleni linaweza kuisha ikiwa wadau wote wakiwamo wazazi, walezi, walimu, viongozi na jamii nzima itasaidia kumlinda msichana.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Salale, Sikudhani Nyambagi anasema kwa sababu msichana anashawishiwa zaidi anapokosa pesa ya mahitaji muhimu ikiwamo taulo za kike, maisha ya gheto hayawafai.

“Mambo mengine wanasababisha wazazi, hivi wasipowapelekea watoto mahitaji muhimu wanadhani nini kitatokea, kazi kubwa tunayofanya huku kwa sasa ni elimu tu,” anasisitiza.



Chanzo: mwananchi.co.tz