Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maisha mapya ya aliyechomwa moto mikono na mama yake

Maisha Pic D Maisha mapya ya aliyechomwa moto mikono na mama yake

Tue, 25 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

“Niko tayari kurudi shule lakini siko tayari kuona wadogo zangu wanakufa njaa, ndio maana naenda kibaruani nipate pesa ili niweze kuwapikia hata mlo mmoja kwa siku.”

Haya ni maneno ya Helena Bahati, mwanafunzi aliyeshindwa kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu baada ya mama yake kumchoma mikono kwa moto.

Baada ya sheria kuchukua mkondo wake na mama yake, Mpipi Emmanuel (33) kukutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano jela, maisha ya watoto hawa sasa yamegeuka shubiri.

Helena (13), sasa anaishi na wadoggo zake wanne pamoja na bibi yao ambaye ni mgonjwa.

Watoto hawa wanaishi kwenye nyumba ndogo pekee iliyopo pembezoni mwa msitu wenye vichaka katika Kijiji cha Shahende wilayani Geita.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili aliyemtembelea nyumbani kwao, Hellena anasema maisha yao yamekuwa magumu kutokana na kukosa msaada, hivyo kujikuta wakila mlo mmoja kwa siku na wakati mwingine kulala njaa.

Anasema tangu mama yake akamatwe na kuwekwa ndani Oktoba 5, mwaka huu yeye amebaki na jukumu la kuhudumia familia na kazi kubwa anayofanya ni kwenda kuomba kazi mashambani na hulipwa Sh 2,000.

“Naamka saa 12 asubuhi naenda shamba, nalima hadi saa tano nalipwa Sh2,000. Hizi nazikusanya zikifika 20,000 nanunua ndoo ya mahindi, nasaga nashirikiana pia na mdogo wangu anayesoma la nne. Kama ndani kuna unga basi nanunua dagaa au kabichi kwa ajili ya mboga,” anasema Helena.

“Bibi anaumwa miguu hawezi kutembea, huwa namuacha na mtoto mimi naondoka. Kukiwa na unga anakoroga uji wanakunywa kabla ya kwenda shule kama hakuna unga basi wataenda hivyo hivyo na siku nyingine hawaendi,” anasema.

Helena anasema kulala njaa kwao ni jambo la kawaida lakini anaumia zaidi anapomuona mdogo wake (miezi tisa au mwaka mmoja) akikosa hata uji na kulia sana nyakati za usiku.

Hellena anasema awali waliishi kwa kumtegemea mama na hawakuwahi kumuona baba yao.

Alivyochomwa moto

Hellena anasema Jumatatu Oktoba 3 mwaka huu, alikwenda shule kuosha dawati kwa ajili ya mtihani na aliporudi nyumbani alimkuta mama yake amekaa nje akiwa na mdogo wake kisha akawahoji kuhusu Sh500 alizosema zilikuwa ndani.

“Tulimwambia mama hatujachukua, akasema hiyo hela ilikuwa ndani mdogo wangu akamwambia mama ungekuwa na hela ungemuomba bibi ya kumnunulia mtoto dawa, si ungechukua yako ukanunue? Mama akasisitiza alikuwa na Sh500 ameweka ndani na hazioni.

“Alafu akaanza kugomba kwanini nimesema kwa mwalimu kuwa ‘mama ameniambia nisifaulu’, nikamwambia mimi sijamwambia mwalimu hivyo na kweli mwalimu mimi sijamwambia kitu kama hicho, akaongea sana usiku tukaenda kulala hakukua na chakula,” anasema.

Mtoto huyo anasimulia kuwa asubuhi saa 12 walipoamka walikuta mlango umefungwa kwa nje, baadaye mama yao akaingia na kuwafunga mikono na kuanza kuwachapa na badaye akawasha moto na kuwachoma wote wawili mikono.

Anasema baada ya tukio hilo, mama yao alipasha maji moto na kuanza kuwakanda maeneo waliyoumia huku kwenye vidonda vya kuungua akiwapaka asali.

“Mama alitoka akaenda kuazima baiskeli ili atupeleke shule lakini mimi na mdogo wangu tuliondoka tukaja kwa bibi na aliporudi nyumbani mdogo wetu mwingine alimwambia tuko kwa bibi, akaja akitaka twende shule bibi alikataa kasema tubaki akihojia kwanini ametuunguza, na mama aliondoka,” anasema

Siku iliyofuata, anasema alikwenda shule kufanya mtihani na mwalimu akamuona amevimba mikono na hawezi kushika kalamu, ndipo alitoa taarifa kwa mtendaji na watu wa Baraza la Mtihani na mama yake akakamatwa na hajamuona tena.

Mtoto huyo anasema pamoja na maumivu aliyoyapata, anajisikia vibaya anapoona wananishi bila mama na hakutarajia kama mama yake anaweza kupewa adhabu ya aina hiyo.

Alipatwa na hasira

Scola Mpipi, bibi mzaa mama wa watoto hao, anasema “mwanangu atakuwa alipatwa na hasira, sikatai watoto wanaadhibiwa ila adhabu hii ilikuwa kubwa na mimi sijawahi kuona, lakini hasira zimemfikisha hapa.

“Tutawatembelea”

Alipoulizwa na Mwanannchi kuhusu hatma ya watoto hao, ofisa ustawi wa jamii mkoa wa Geita, Frank Moshi alisema afisa mwenzake ngazi ya wilaya atawatembelea na kufanya tathmini ili kujua ndugu walipo na uwezo wao; kisha kujadiliana kuhusu namna ya kuwatunza watoto hao, kwa kuwa ni jukumu lao.

Kuhusu mtoto mdogo aliyekuwa akinyonya, Moshi alisema afisa ustawi wa jamii husika atawezesha mtoto huyo kuunganishwa na mama yake ili aendelee na haki ya kupata maziwa ya mama kwa muda unaoshariwa na wataalamu wa afya.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Geita Wilson Shimo amesema viongozi wa kijiji husika wanawatambua ndugu wa mwanamke huyo na kitakachofanyika ni kuwaunganisha nao ili waweze kuendelea na maisha kama watoto wengine.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live