Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maisha kamili ya mwanafunzi aliyekatisha uhai wake kwa risasi

44151 Jasmine+pic Maisha kamili ya mwanafunzi aliyekatisha uhai wake kwa risasi

Thu, 28 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. “Ni mtoto asiyewajua wazazi wake na asiyejua kazaliwa wapi? mtoto huyu anatamani kukiona kifo chake wakati wowote, mtu yeyote atakayesoma shajara (daary) hii ndiye atakayeandika siku ya kifo chake”.

Huo ni ujumbe uliouachwa na mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Lupanga, Jasmin Ngole.

Jasmin (18) alijiua kwa kujipiga risasi kwenye koo na kufumua sehemu ya utosi.

Kifo chake kimeacha maswali mengi kutokana kauli zake kabla ya kujiua na ujumbe aliouandika kwenye shajara aliyomkabidhi rafiki yake, Imelda Milanzi siku moja kabla ya kujiua.

Jinsi ilivyokuwa

Februari 19, mwaka huu, saa 11 alfajili, eneo la Kola B’ Manispaa ya Morogoro mwili wa Jasmin ulikutwa kando mwa barabara huku bastola aliyotumia kujiua, mali Profesa Hamis Maige yenye magazine moja na ganda la risasi ikiwa pembeni yake.

Baada ya uchunguzi wa kidaktari mwili wa Jasmin ulizikwa Machi 21, katika makaburi ya Kola, Morogoro huku mazishi yake yakihudhuriwa na mamia ya watu wakiwamo wanafunzi wenzake.

Profesa Mahige amekiri mbele ya polisi kuwa mmiliki wa bastola hiyo.

Imelda aliyekuwa rafiki wa karibu wa Jasmin na kusoma naye darasa moja, anaeleza kwamba anamfahamu tangu wakiwa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Kigurunyembe Mazoezi na tangu hapo wakawa marafiki mpaka walipofaulu na kuchaguliwa kidato cha kwanza Lupanga.

Anasema siku moja kabla ya kifo chake, Jasmin alifika nyumbani kwao ambapo mbali na mazungumzo alimkabidhi shajara, kitabu cha shule, fedha taslimu Sh10,000 kama zawadi na Sh10,000 nyingine kwa ajili ya kumlipia madeni anayodaiwa shuleni na kadi ya Valentine. Akielezea namna alivyomkabidhi shajara hiyo, Imelda anasema ilikuwa saa mbili usiku Jasmin alipofika nyumbani hapo maeneo ya Bigwa na baada ya muda mfupi wakiwa wanazungumza alimkabidhi vitu hivyo akiwa ni mwenye furaha.

Anasema hakuifungua shajara hiyo kwa muda ule kwani hakuwa na mashaka yoyote kwa kuwa Jasmin alikuwa katika hali ya kawaida na huwa akimzawadia vitu mbalimbali.

Baadaye saa tatu usiku huo, Jasmin aliaga na akumsindikiza mita chache na kumuacha akiendelea na safari.

Siku iliyofuata Imelda anasema akiwa darasani aliona polisi wamefika shuleni hapo na baada ya muda walimu walimuita mbele ya polisi hao ambao walimuuliza kama anafahamu kitu chochote kuhusu kifo cha Jasmin na hapo ndipo alipogundua rafiki yake amejiua kwa risasi.

Baada ya kuhojiwa na polisi anasema alitoa shajara hiyo na baada ya kuifungua ndipo walipogundua imeandikwa ujumbe huo, alichukuliwa na kupelekwa polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi kisha aliruhusiwa kurudi nyumbani.

“Ule ujumbe aliandika Jasmin mwenyewe, ninautambua mwandiko wake kwa sababu mara nyingi huwa tunaandikiana kazi za darasani, mpaka sasa daary iko polisi,” anasema Imelda.

Imelda anasema Jasmin alikuwa na tabia ya kuzungumzia masuala ya kifo chake na mara nyingi alikuwa akisema kimekaribia na kwamba kitakuwa kibaya kiasi cha watu kushindwa kuuaga mwili wake.

Huku akibubujikwa machozi, Imelda anasema siku moja kabla ya kujiua Jasmin alikwenda shuleni akiwa na Sh10,000 na kumwambia yeye na wanafunzi wenzake wale wanachokitaka naye alilipa akiwa na furaha.

Kuhusu maendeleo kitaaluma ya rafiki yake huyo, anasema yalikuwa ya wastani na kwamba alikuwa na mahudhurio mazuri shuleni huku akiwa mwepesi kushiriki katika michezo shuleni.

Aidha, Imelda anasema katika uhai wake Jasmin aliwahi kumweleza kuwa yeye ni yatima na kwamba analelewa na Profesa Mahige ambaye anamwita shemeji. Hata hivyo, kumwmbia kama ama Profesa anamiliki au yeye (Jasmin) anaweza kutumia silaha.

Imelda anasema baada ya kupata taarifa za kifo cha rafiki yake alipata mshtuko kiasi cha kushindwa kufanya mitihani ya mwezi iliyofanyika siku moja baada ya shughuli za mazishi.

Makamu Mkuu wa shule ya Sekondari Lupanga, Mwalimu Daud Masunga, anasema Jasmin alikuwa mcheshi, mwenye nidhamu na aliyependa kushirikiana na wenzake na kwamba hajawahi kupokea malalamiko kutoka kwa walezi wala wanafunzi wenzake kuhusu mwenendo wa Jasmin kitabia.

Kwa upande wake Profesa Mahige alishindwa kueleza namna tukio hilo lilivyotokea isipokuwa binti yake Zakia Mahige anasema siku hiyo Jasmin alirudi kutoka shule na kuendelea na shughuli za nyumbani na jioni alimuogesha mtoto mdogo wa Profesa kisha kumuingiza chumbani kwa ajili ya kumvalisha nguo.

Anasema baadaye mtoto huyo alitoka akiwa mtupu na alipoulizwa kwa nini hajavaa nguo alisema dada (Jasmin) katoka nje.

“Kadri giza lilipozidi kuingia Jasmin hakuonekana nyumbani na hakukuwa na taarifa zilizoeleza wapi alipo jambo ambalo lilimtia wasiwasi baba (Profesa Mahige) na kuanza kumtafuta na kutoa taarifa kwa watu aliozani wangeweza kumsaidia kumpata,” anasema Zakia.

Anasema baadaye Profesa alimpigia simu mama mlezi wa Jasmin ambaye aliwahi kuwa mke wake na kumpa taarifa za kupotea kwa binti huyo huku akiendelea kumtafuta.

Binti huyo anasema kuwa asubuhi Profesa alipata taarifa kuna mwili wa msichana umekutwa eneo la Bigwa ukiwa na jeraha hivyo aliamua kwenda kushuhudia na alipofika alikuta ni wa Jasmin, ukiwa umelala chini pembeni kukiwa na bastola ambayo aliitambua mbele ya polisi kuwa ni mali yake.

“Baada ya baba kuutambua mwili wa Jasmin na bastola yake, polisi wakamchukua na kuondoka naye kituoni kwa ajili ya mahojiano, alikaa huko kwa siku moja na baadaye walimtoa kwa dhamana,” anasema Zakia.

Anasema waliishi na Jasmin kama ndugu yao na hata alipokosea walikuwa wakimuonya kwa kuzungumza naye kama ambayo mtoto mwingine anaonywa, hivyo uamuzi wa kujiua umewaumiza na kuwahuzunisha.

Christina Makinda ambaye ni mama mlezi wa Jasmin anasema kwa sasa anaishi Luangwa, Lindi na aliondoka mkoani Morogoro Oktoba mwaka jana akimuacha Jasmin nyumbani kwa Profesa kwa kuwa alikuwa anaingia kidato cha nne, hivyo hakutaka kumsumbua kimasomo.

Christina anasema aliwahi kupata taarifa kutoka kwa profesa Maige akimwelezea Jasmin kubadilika kitabia, naye aliwahi kuzungumza naye mara kadhaa na kumhoji kwa nini amebadilika, lakini binti huyo hakuwa na majibu.

Anasema inadaiwa binti huyo alikuwa na tabia ya kutoroka mara kwa mara, hata hivyo alikuwa akirejea nyumbani na alipokuwa akiulizwa hakuwahi kusema alikokuwa.

Mbali na kuzungumza naye, Christina anasema aliwatumia walimu taarifa za mabadiliko ya kitabia ya Jasmin ili aweze kupata msaada wao kwa kumuonya na kufuatilia mienendo yake.

Anaeleza kuwa alimchukua na kumlea Jasmin kutokana na kifo cha mama yake muda mfupi baada ya kumzaa.

Anasema mama wa Jamin hakueleza, kuonesha wala kutoa taarifa zilizohusiana na mwanaume aliyempa ujauzito.



Chanzo: mwananchi.co.tz