Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahiza awapa tano Polisi ukamataji ‘watoto wa ibilisi’

Mahiza Pic Ibilisi Data Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Mwantumu Mahiza

Sun, 7 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Mwantumu Mahiza amelipongeza Jeshi la Polisi mkoani Tanga kwa kuwakamata vijana 117 maarufu watoto wa ibilisi wanaofanya matukio ya kuwapora watu, kuwapiga na kuwajeruhi kwa kutumia mapanga.

Watoto hao wa ibilisi wanaofanya matukio hayo wa naumri wa kuanzia miaka 12 hadi 18 wengi wakiwa ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Mahiza ambaye na yeye alishawahi kuvamiwa nyumbani kwake mwaka jana na vijana hao amesema wapovamia nyumbani kwake walikata mfumo wa umeme na kisha kuiba televisioni na music system.

''Binafsi nimefurahi kukamatwa kwa watoto hao kwa kila walichonifanyia mwaka jana, vijana hawa wamekuwa ni kero kubwa kwa wakazi wa Jiji la Tanga, watu hawalali , ukitembea usiku na ukakutana nao kwa kweli huna bahati," amesema Mahiza.

Amesema Jiji la Tanga lilikuwa limepoteza amani kutokana na watoto hao, hatua ambayo polisi wameichukua ni ya kuungwa mkono na kila mwananchi.

Amesema wazazi wana wajibu mkubwa wa kuwafundisha watoto wao maadili mema, na wasikwepe wajibu huo.

Amewashauri wananchi kutonunua vitu mkononi kwa kuwa vingi ndio vile vinavyopatikana kwenye matukio ya uhalifu hiyo ikiwa ni njia mojawapo ya kukabiliana na uhalifu wa aina hiyo.

Mahiza amesema wazazi ambao watoto wao wanakamatwa wakihusishwa na vitendo hivyo nao wawajibishwe kwa kushindwa kuwalea watoto wao kwenye maadili mema.

Mahiza ambaye alishawahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga na naibu Waziri wa Elimu amelitaka jeshi la polisi kuendelea na kazi ya kutunza amani lakini pia kuendelea kupambana uhalifu mwingine ikiwemo matumizi wa dawa za kulevya, uhamiaji haramu na ukahaba .

Amemtaka kamishna wa Scauti mkoa wa Tanga na Wilaya ya Tanga kusaidia kufundisha maadili shuleni.

Meneja wa kituo cha Sayansi Tanga, Gipson Kawago akizungumzia watoto hao amesema alikutana nao siku moja barabarani na walimvamia wakiwa na mapanga na kuanza kumshambulia.

Kawago amesema baada ya kumvamia walianza kuchukua simu na kisha wakaanza kutumia mapamba kumpiga huku akipiga kelele akihitaji msaada kutoka kwa raia wema.

Mfanyabiashara wa Mkonge Tanga, Aisha Rugarabamu amesema operesheni ya watoto wa ibilisi imesaidia kuwajua wezi waliomuibia mwaka 2019.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoawa Tanga, ACP Safia Jongo alisema wamekamata watoto wa ibilisi 117 kutokana na oparesheni iliyoendelea iliyoanza Oktoba mwaka huu.

"Nimetoka Tabora mahali ambapo kulikua na watoto wanaojiita Roho Saba nikamalizana nao, nimekuja Tanga nimekuta watoto wanajiita Ibilisi, watoto wenye umri wa wa miaka 12 hadi 18 ngoja tuendelee nao lakini nataka niwahakikishie kuwa mkoa wa Tanga sio wa kuchezea," alisema Kamanda Jongo.

Chanzo: mwananchidigital