Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahenge aingilia kati mgogoro viwanja 170

Bfad76e3dde2037907a2de9878fdc538 Mahenge aingilia kati mgogoro viwanja 170

Thu, 12 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk Bilinith Mahenge ametoa siku 14 kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutoa orodha ya wamiliki wa viwanja 170 vilivyopimwa na kutolewa hati katika eneo la Chigongwe ili kuondoa mgogoro uliopo kati yake na Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG).

Alitoa agizo hilo jana mara baada ya kutembelea eneo hilo ambalo kanisa la TAG liliomba ekari 200 kwa ajili ya kufanya uwekezaji.

Dk Mahenge alisema kumekuwa na mkanganyiko kutokana na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) kuanza kupima eneo hilo na baada ya CDA kufutwa Jiji likaendelea na upimaji huku mambo ya TAG yakiwa bado hayajatekelezwa.

"Awali TAG waliomba ekari 200 lakini inaonekana eneo hili lilikuwa na ukubwa wa zaidi ya ekari 600 ndipo walipopima viwanja na vikauzwa, lakini ukiangalia kuna kama ekari 150 ambazo hazijapimwa, kama TAG watakubali kuchukua eneo hilo wanaweza kufanya hivyo na kama wataona haliwatoshi kwa ajili ya shughuli zao watapatiwa eneo lingine," alisema.

Alisema hakuna ubishi kuwa yapo makosa ambayo yalifanywa na baadhi ya watendaji wa CDA wakati TAG wakifuatilia eneo hilo.

"Natoa siku 14 nipate orodha ya wamiliki 170 wa viwanja vilivyopimwa katika eneo hili ambao walipata hati na hizo hati tuzione tuthibitishe kama eneo hilo lipo,"alisema.

Hata hivyo baada ya eneo hilo kupimwa viwanja viliuzwa kwa wananchi na baadhi ya taasisi kutokana na mkanganyiko uliokuwepo juu ya ukubwa wa eneo.

Happiness Mgalula ambaye ni Katibu tawala msaidizi wa Miundombinu alisema TAG waliomba ekari 200.

"Yapo mapungufu yaliyofanywa na CDA na eneo ambalo limepimwa ni ekari 386 na kupatikama viwanja 170 ambavyo waliuziwa wananchi na kupatiwa hati,"alisema.

Alisema watatekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa la kutaka eneo lililobaki kupimwa na kujulikana limebakia kiasi gani.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Josephat Maganga alitaka busara kutumika katika kuamua jambo hilo.

Alisema wataalamu wa jiji lazima wajiridhishe ukubwa la eneo ambalo halijapimwa ili maamuzi yaweze kutolewa.

Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la TAG, Steven Mahinyila ambaye ni Askofu wa Jimbo la Dodoma, alisema mwaka 2009 TAG ilifika eneo la Chigongwe kuomba eneo la kujenga chuo kikuu na walipewa masharti ya kukarabati madarasa na kuchimba kisima masharti ambayo waliyatimiza.

Alisema baada ya kutekeleza walirudi serikali ya kijiji ambapo waliambiwa kama wanahitaji zaidi ya ekari 50 hawana mamlaka lakini waliandikiwa barua ya kuwatambulisha CDA.

Alisema ilipofika mwaka 2011 Katibu wa kanisa hilo aliandika barua kwenda CDA na waliweza kwenda kwenye eneo hilo wakiwa na wataalamu wa CDA, baada ya eneo kupimwa ilionekana lina ekari 560 sio ekari 200 na waliambiwa waainishe mradi gani wanataka kuweka eneo hilo.

“Mei 2013 walipeleka andiko la mradi CDA na walianza kufuatilia lakini baadaye tukaitwa mahakamani kwa kushindwa kulipa wananchi fidia na waliofungua kesi ni wananchi kutoka Nala na Chigongwe bila kupitia serikali ya vijiji.

"Tuliweka mwanasheria lakini waliotushtaki hawakuonekana mahakamani na hatimaye kesi hiyo ilifutwa na tukaendelea kufuatilia suala hilo CDA lakini baada ya CDA kuvunjwa tukarudi Jiji na kwenda Wizara ya Ardhi ambapo walisema turudi Jiji ndio wahusika," alisema.

Mchungaji Mahinyila alisema wameendelea kufuatilia suala hilo bila mafanikio na ndipo Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk Barnabas Mkosamali alipotoa ombi hilo mbele ya Rais John Magufuli alipokwenda kufunga mkutano wa maaskofu Jijini Dodona na walimuomba kusaidia ili kanisa hilo kupatiwa eneo waliloomba.

"Ombi alilotoa mkuu wa mkoa la kutaka kanisa kukubali ekari 150 zilizopo tutaliwasilisha kwa Askofu Mkosamali na tutaleta majibu kwako," alisema.

Naye, Chaula Ameri kutoka Idara ya Mipango Miji alisema kumbukumbu zinaonesha kijiji kilikuwa na ekari 200, kilitambulisha TAG kwa CDA na ushahidi wa barua upo.

Alisema wataalamu wa ardhi walipofika na kupima waligundua kuwa eneo hilo halina ekari 200 kama ilivyoelezwa bali lilikuwa ni ekari 560 na ndipo CDA ikatoa barua kwa TAG ya kutaka mpango wa matumizi ya eneo lile na hakuna kilichoendelea baada ya barua hiyo kwani kumbukumbu hazioneshi kama mpango ulipelekwa.

"Baadae baada ya kuja kupima tena eneo hili kwa kutumia GPS tuligundua eneo lina ekari 635.7," alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz