Mwanza. Washtakiwa 10 kati ya 12 wa kesi ya dhahabu kilo 35.34 yenye thamani ya Sh2 bilioni iliyokamatwa nchini Kenya na kurudishwa Tanzania wamefutiwa mashtaka yao.
Hatua hiyo imefikiwa leo Alhamisi Septemba 5, 2019 baada ya kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza mbele ya Hakimu Mkazi wa Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Rhoda Ngimilanga.
Wakili wa Serikali, Shedracky Kimaro ameieleza Mahakama kwamba Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) nchini Tanzania hana nia ya kuendelea na kesi dhidi ya washtakiwa hao 10.
Amejielekeza katika kifungu cha 91 (1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kuwafutia mashtaka washtakiwa hao.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Ngimilanga amesema mahakama inawaachilia huru.
"Mahakama imewafutia mashtaka washtakiwa 10," amesema Hakimu Ngimilanga.
Habari zinazohusiana na hii
- Washtakiwa wanne kati ya 12 wa kesi ya kusafirisha dhahabu wakiri kosa
- Washtakiwa kesi ya dhahabu wakacha kifungo, walipa faini