Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yaonyeshwa miamala ilivyoingia kesi ya kina Dk Pima

Md Pima Mahakama yaonyeshwa miamala ilivyoingia kesi ya kina Dk Pima

Thu, 23 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imeelezwa jinsi fedha zilivyoingia, kutoka kwenye akaunti za watuhumiwa wa kesi ya uhujumu uchumi ikiwemo Sh103 milioni zilivyoingizwa kwenye akaunti ya aliyekuwa Mchumi wa Jiji la Arusha, Innocent Maduhu.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5/2022 mbali na Maduhu watuhumiwa wengine ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji hilo Dk John Pima na aliyekuwa Mwekahazina wa jiji hilo Mariam Mshana, watuhumiwa ambao wanakabiliwa na makosa tisa ikiwemo utakatishaji fedha Sh103 milioni.

 Leo Jumatano Februari 23, 2023 shahidi wa 23 wa Jamhuri katika kesi hiyo, Msaidizi wa Meneja wa huduma kwa wateja kutoka Benki ya NMB Tawi la Clock Tower Arusha, Peter Mlelwa ameeleza kuhusu miamala hiyo iliyoingia na kutoka kwenye akaunti binafsi za watuhumiwa hao.

Akiongozwa kutoa ushahidi na Wakili wa Serikali mwandamizi, Timotheo Mmari, shahidi huyo alidai kuwa Septemba 9,2022 alipokea barua kutoka kwa Ofisa wa Takukuru Ramadhan Juma, aliyekuwa akitaka taarifa za kibenki (bank statement) za Dk Pima, Mariam na Maduhu katika akaunti zao binafsi.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Serafini Nsana anayesikiliza kesi hiyo, shahidi huyo alidai kuwa siku hiyo aliweza kuchapisha taarifa za Dk Pima na Mariam huku ya Maduhu ikichapishwa Oktoba 12, 2022.

Akitumia taarifa hizo kutoa ushahidi mahakamani hapo amedai katika taarifa ya Maduhu, inaonyesha Machi 28, 2022 miamala miwili ikiwemo wa kutoa Sh10 milioni katika Tawi la NMB Clock Tower pamoja na muamala wa Sh103 milioni ulioingia katika akaunti yake ikitokea LGA Development Account BoT.

Amedai kuwa kabla ya muamala huo kuingia, akaunti hiyo ilikuwa na Sh5.7 milioni huku Machi 29, 2022 Sh75 milioni ilitolewa katika Tawi la Makole Business Center na kuwa muamala wa kuhamisha fedha kwenda kwenye akaunti nyingine ya Maduhu wa Sh25milioni ukifeli na kurudi kwenye akaunti hiyo.

Shahidi huyo aliendelea kuieleza mahakama kuwa Aprili mosi 2022, ikifanyika miamala minne ikiwemo wa kuhamisha fedha Sh17 milioni zilizohamishwa kwenda kwa Anna Kulaya na Aprili 11, 2022 akihamisha Sh3.5 milioni zilizotumwa kwenye akaunti ya Fau Motors.

Kuhusu akaunti ya Dk Pima, alidai kuwa Machi 29,2022 ilifanyika miamala miwili ukiwemo wa Sh10 milioni zilizoingia kutoka NMB tawi la Mazengo, Dodoma.

Kuhusu taarifa ya Mariam, inaonyesha Machi 28, 2022 aliwekewa muamala mmoja wa Sh5 milioni kutoka Tawi la Clock Tower, Machi 29 Sh 1.5 milioni zinawekwa na Mariam mwenyewe katika Tawi la Makole Business Center Dodoma na Sh18.9 ikiingia kutoka LGA General Fund.

Shauri hilo limeahirishwa hadi kesho Alhamisi litakapoendelea kusikilizwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live