Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yaelezwa Lissu anaendelea na matibabu

68119 Lissu+pic

Wed, 24 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mdhamini wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa mshtakiwa huyo bado anaendelea kupatiwa matibabu nchini, Ubeljiji.

Mdhamini huyo, Robert Katula, ameieleza mahakama hiyo leo Jumatano Julai 24, 2019 , mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

Lissu na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Katula amedai amepewa taarifa kuwa, Lissu bado anaendelea na matibabu.

Mshtakiwa huyo, yupo nje kwa ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi, Septemba 7 mwaka 2017 jijini Dodoma.

Awali, wakili wa Serikali, Slyvia Mitato amedai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa, hivyo kutokana na mshtakiwa mmoja kuwa mgonjwa, aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Pia Soma

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 22, 2019  itakapotajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Mbali na Lissu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya jinai namba 208/2016 ni Mhariri wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.

Washtakiwa hao kwa pamoja  wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

Katika shtaka la pili wanadaiwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob anadaiwa Januari 13 ,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Inadaiwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Chanzo: mwananchi.co.tz