Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yaamuru mwili wa bilionea wa Tanzanite uzikwe

39606 Pic+billionea Mahakama yaamuru mwili wa bilionea wa Tanzanite uzikwe

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hatimaye mvutano wa maziko ya mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite, Jubilate Ulomi umekwisha baada ya Mahakama ya Wilaya ya Hai kutengua amri yake ya zuio la maziko hayo na kuamuru familia iendelee na utaratibu.

Amri ya kutengua zuio hilo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi, Devota Msoffe ikiwa ni siku ya 17 tangu mfanyabiashara huyo alipofariki dunia.

Awali, Mahakama ilizuia maziko ya Jubilate baada ya kupokea maombi yaliyofunguliwa na Zainabu Rashidi aliyedai kuwa ni mke wake halali, ambaye aliomba maziko yasifanyike hadi ufanyike uchunguzi wa chanzo cha kifo.

Pia, aliomba apatiwe idhini ya kuzika kwa madai kuwa ndiye mwenye haki, maombi ambayo yalipingwa na familia ya Jubilate iliyodai kuwa hawamtambui kama mke halali wa ndugu yao.

Awali, shauri hilo lilipangwa kutajwa mahakamani hapo Februari 7, lakini hata kabla ya tarehe hiyo kufika, jana mahakama hiyo iliamua kutengua amri yake ya zuio na kuiruhusu familia kuendelea na maziko hayo.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Msoffe alisema hana sababu ya kusubiri hadi tarehe hiyo kwa kuwa uchunguzi wa chanzo cha kifo umeshafanyika na taarifa yake imeshatolewa.

“Nakubaliana na hoja za mawakili wa walalamikiwa na ninatengua amri zilizotolewa Januari 22, zinazowazuia ndugu kumzika Jubilate,” alisema Hakimu Msoffe.

Jubilate aliyekuwa mchimbaji na mmiliki wa migodi kadhaa ya madini ya Tanzanite huko Mirerani mkoani Manyara, alifariki dunia Januari 15 katika Hospitali ya Aga Khan ya jijini Nairobi, Kenya.

Soma zaidi: Mwili wakwama mochwari siku saba kisa mvutano wa mke na ndugu wa marehemu



Chanzo: mwananchi.co.tz