Mahakama Kuu ya Tanzania imeliamuru Gazeti la The Citizen kumlipa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu kiasi cha Tsh bilioni 2.5 kwa kuandika habari iliyomchafulia jina lake.
Katika adhabu hiyo, Tsh bilioni 2 ni kwa ajili ya kumlipa fidia kwa kuchafulia jina na kumshushia hadhi yake.
Hukumu hiyo imetolewa leo Mahakama Kuu, Masijala ya Dar es Salaam, ikielezwa kuwa gazeti hilo lilichapisha taarifa ambazo zilimtuhumu Mchechu juu ya matumizi mabaya ya fedha za umma na kutumia maneno yaliyoshusha hadhi yake, huku wakidai walinukuu maneno ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati Dkt. John Magufuli alipokuwa akizindua mradi wa nyumba za NHC zilizopo Dodoma mwaka 2017.
Mchechu ambaye wiki iliyopita aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Msajili wa Hazina, alifungua kesi hiyo mwaka jana katika Mahakama Kuu ya Tanzania akilitaka gazeti la The Citizen kumlipa fidia ya Sh. bilioni 3 kwa madai ya kuandika habari zilizomchafua.
Katika kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa Mei 13, 2022 mbele ya Jaji Leila Mgonya wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Mchechu alidai toleo la Gazeti hilo la Machi 23, 2018, lilichapisha habari iliyosomeka ‘Why JPM dissolved NHC Board, sacked Mchechu’ ikiwa na tafsiri isiyo rasmi kuwa kwanini JPM alivunja Bodi ya NHC, kumfukuza Mchechu’.
“Habari hii ililenga kunichafua, kunishushia hadhi, kunikosanisha na jamii kubwa ya Watanzania na kuonekana kuwa ni mimi ni mtu nisiyefaa kabisa kuwa kiongozi au sehemu ya jamii njema ya Watanzania mtu nisiye na maadili, nisiyeaminika na kimsingi nisiyestahili hata kuongoza popote,” alisema Mchechu ambaye anawakilishwa na mawakili wa kujitegemea Aliko Mwamanenge na Vitalis Peter katika kesi hiyo.
Mchechu ambaye alirejeshwa katika nafasi yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan baada ya kuondoka mwaka 2018, alisema habari hiyo ina upotoshaji wa kimantiki na kimaudhui kwa kuwa hajawahi kufukuzwa kazi kama ilivyodaiwa.
“The Citizen liliandika habari ile likijua sijafukuzwa kazi na wala Mheshimiwa Rais (John Magufuli) hakuwahi kunifukuza kazi na hii ilikuwa ni habari ya uongo na yenye nia ovu ya kunichafua na kunishushia hadhi katika familia yangu, taifa na duniani kwa ujumla,” alisisitiza Mchechu.
Awali ilidaiwa kuwa katika habari hiyo iliyokuwa kubwa kwenye ukurasa wa mbele ilisema Mchechu alikuwa akichunguzwa na Bodi ya NHC na kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), juu ya mgongano wa kimaslahi ya utafutaji na upatikanaji wa ekari 500 za mradi wa NHC wa Safari City jijini Arusha.
Ardhi hiyo iliripotiwa kununuliwa na kampuni inayomilikiwa na Mchechu kutoka kwa raia wa kigeni ambapo uchunguzi ulionyesha aliiuzia NHC kwa bei ya juu huku pia akidaiwa kumtumia mkandarasi wa NHC kutengeneza barabara kwenda kwenye eneo lake lililo karibu na eneo la mradi wa Safari City kwa gharama za shirika.
Taarifa hiyo pia ilidai kuwa kampuni ya PHILS International ya Dubai ilipewa kazi katika mradi wa Kawe kwa uamuzi wa Mchechu bila kumhusisha Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi cha NHC, Hamis Mpinda na kwamba uchunguzi ulikuwa unafanywa kuhusu madai ya kampuni ambayo mke wa Mchechu ni mkurugenzi kwa kupewa mkataba wa kutoa bima kwa ajili ya nyumba za shirika mkoani Mtwara jambo ambalo ni kinyume cha kanuni za utumishi wa umma.
Aidha habari hiyo ya gazeti la The Citizen ilidai vyanzo vya habari vilibainisha kuwa kamati iliyoundwa kuchunguza matumizi mabaya ya ofisi ndani ya Shirika la Nyumba NHC ulionyesha ukiukwaji na matumizi mabaya ya fedha za umma madai ambayo yamekanushwa na Mchechu.
“Habari hii haina hata chembe ya ukweli isipokuwa ililenga kunichafua na kuniharibia heshima yangu niliyoijenga katika jamii kwa muda mrefu na wala NHC haijawahi kununua ekari 500 jijini Arusha kwa ajili ya mradi wa Safari City bali ekari halisi ni 583 na sijawahi kuchunguzwa kutokana na bodi ya shirika au taasisi yoyote ya uchunguzi ikiwamo TAKUKURU kuhusu mradi huo na sina ardhi karibu na mradi huo kama ilivyodaiwa” alifafanua Mchechu.
Aliongeza kuwa ardhi anayodaiwa kuiuzia NHC ni taarifa za uongo kwani hajawahi kumiliki ardhi mkoa wa Arusha katika maisha yake na wala hana kampuni iliyowahi kufanya hiyo na haajawahi kuiuzia NHC ardhi popote nchini Tanzania na wala hawajahi kuingilia masuala ya ununuzi akiwa mtendaji mkuu wa shirika na wala kupoka mamlaka hayo.
Kuhusu madai ya kampuni ya mke wake akisema halijawahi kufanyika jambo kama hilo na kwamba NHC haikati bima kwa ajili ya mali zake zikiwamo nyumba, na kwamba suala la uchunguzi wa matumizi mabaya ya ofisi na fedha za umma ni uongo kwakuwa hakujawi kuwa na taarifa ya uchunguzi iliyomtia hatiani kwa jambo hilo wala ukosefu wa maadili.
Kufuatia habari hiyo Mchechu amesema licha ya kumshushia hadhi pia alikosa kuaminika hivyo kupoteza nafasi nyingi za kibiashara alizokuwa anafanya pamoja na kuondokewa na wabia katika kampuni ambazo ana uhusiano nazo kibiashara.
“Taarifa hii ilinisababishia mfadhaiko mkubwa wa akili, msongo wa mawazo hofu na kudhuru afya yangu na ilinipotezea nafasi ya maendeleo yangu kikazi na kunipotezea mapato ya ajira yangu na ushiriki wangu katika bodi mbalimbali ndani na nje ya nchi,” alifafanua.
Mbele ya Mahakama Mchechu alidai wakati habari hiyo inaandikwa alikuwa katika mchakato wa kupata nafasi ya ofisa mtendaji mkuu wa taasisi ya kimataifa ya kifedha ya Shelter Afrique hivyo kusababisha kuikosa licha ya kwamba alikuwa akiongoza huku nafasi yake ya uongozi ikiingia doa kwa hofu ya usalama wa sadaka za waumini katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani akiwa kama Mwenyekiti wa Halmashauri ya Fedha.
“Habari hii imenifanya nionekane mlafi, tapeli, mlanguzi, mtu anayetumia vibaya nafasi yake lakini pamoja na mambo mengine naiomba mahakama nisafishwe na chombo hiki na nilipwe fidia kutokana na athari na hasara nilizopata,” alidai Mchechu.