Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama kuu yampa haki ya kusimamia mali za bilionea Olomi mjane na mtoto

60210 Pic+olomi

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, imetupilia mbali maombi ya Werandumi  Olomi, mdogo wa Bilionea Jubilate  Olomi kusimamia na kukusanya yeye pekee mali za bilionea huyo, na kuwapa haki hiyo watu watatu.

Watatu hao ni mjane wa marehemu, Zainabu Rashid na mtoto wa marehemu, Julius  Olomi  na Werandumi.

 Bilionea Olomi  aliyefariki  Januari 15  mwaka huu, katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya, ameacha migodi ya Tanzanite iliyoko Mirerani, nyumba za kifahari zilizoko Arusha na Mirerani, mashamba, magari na mali kadhaa.

Akisoma hukumu katika kesi hiyo, Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Maimbari Frank  kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa hiyo Kanda ya Moshi, Dk Fauz Twaib, amesema Mahakama imetupa maombi ya Werandumi kwa lengo la kulinda maslahi ya pande zote hasa watoto watatu wa marehemu.

Jaji Twaib amesema awali, Werandumi aliyekuwa anatetewa na Wakili Joseph Ngiloi, aliwasilisha maombi ya kutaka kuwa msimamizi wa muda wa mali za marehemu lakini alipingwa na mjane, Zainabu Rajabu aliyezaa watoto wawili na bilionea huyo  na mtoto mwingine wa  marehemu Julius Olomi.

 

Pia Soma

Amesema kwa kuzingatia kifungu  cha 23 cha sheria ya usimamizi wa mirathi kutokana na uamuzi huo, hakuna chochote ambacho kitafanyika juu ya mali za bilionea huyo ambaye alikuwa anamiliki migodi ya Mirerani, nyumba mbili, moja Arusha na nyingine Mirerani pamoja na mashamba na mali kadhaa bila makubaliano ya pande zote mbili.

Jaji, Twaib amesema ili kufikia utekelezaji wa hukumu hiyo, kila mmoja anapaswa kuhakikisha amesaini nyaraka muhimu za Mahakama na uamuzi kuhusu mali a marehemu Jubilate yatafanywa kwa maandishi hadi kesi ya msingi ya usimamizi wa mirathi itakapotolewa uamuzi.

Jaji Twaib alitaka pande hizo kukubaliana katika kila jambo na kama wameshindwa kukubaliana kwa kuzingatia Sheria ya Mirathi, anaweza kuteuliwa mtu mwingine kutoka  ofisi ya kabidhi Wasihi  Mkuu wa Serikali kusimamia na kukusanya mali za marehemu.

Amesema msingi wa uamuzi huo unatokana na ukweli kuwa marehemu aliacha watoto watatu ambao watahitaji matunzo kutokana na mali za baba yao, hivyo anapaswa kuwapo mtu ambaye atasimamia haki za watoto hao.

Akizungumzia hoja ya Werandumi kuwa alikuwa akimiliki kwa pamoja na marehemu Jubilate migodi ya Mirerani na kuna wafanyakazi ambao wanadai, amesema hoja hiyo imekosa uthibitisho kwa sababu imepingwa pia na mjane na mtoto wa marehemu.

“Mahakama ilifikia hatua ya kumuita Mkuu wa Polisi wa Mirerani,  SP Evalist Makala ili kuisaidia juu ya hoja kuwa, wakati marehemu anaumwa mgodi ulikuwa unafanya kazi ama la, lakini shahidi huyo alishindwa kuisaidia,” amesema.

 

Hata hivyo, amesema Mahakama imepokea kielelezo RS/7 ambachoo shahidi, Saimon Mayalawa  alieleza kuwa mgodi ulikuwa umesimama wakati wote marehemu alipokuwa mgonjwa na hivyo, hakuna malipo yaliyofanywa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Jaji Twaib hata hivyo, amesema watu waliopewa haki ya kusimamia na kukusanya mali za marehemu wataendelea kupata msaada wa kisheria kutoka kwa mawakili wao hadi shauri la usimamizi wa mirathi litakapomalizika.

Awali,  kabla ya mgogoro huo haujafikishwa  mahakamani, uliibuka mgogoro wa kugombea mwili na kutaka kuzika ambao ulifikishwa kwa  Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na baada ya kushindwa kuelewana pande zote, alishauri ufikishwe mahakamani na ndugu wa Olomi walipata haki ya kuzika.

Wakizungumza baada ya uamuzi huo, mawakili Ngilio na  Engelberth Boniphace aliyekuwa anamtetea Mjane na mtoto wa marehemu, walieleza kukubaliana na uamuzi wa Mahakama.

Wakili Boniphace alisema ni mzuri na umelenga kuondoa mgogoro katika familia zote kabla ya kuamuliwa kesi ya msingi ya nani atakuwa msimamizi wa mirathi.

Wakili Ngiloi alisema uamuzi huo utasaidia kulinda mali za marehemu kwa sababu zitakuwa katika mikono salama.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz