Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni (Kinondoni) itaanza kufanya uchunguzi wa chanzo cha kifo cha mwanamke aliyedaiwa kufia mahabusu katika kituo cha Polisi Mburahati, Stella Moses kuanzia Februari 17, mwaka huu.
Mahakama hiyo imewaita wadaawa katika shauri la maombi ya uchunguzi wa chanzo cha kifo hicho ikiwataka kufika mahakamani hapo tarehe hiyo kwa ajili ya kuanza uchunguzi huo.
Wakili wa familia ya marehemu Stella, Peter Madeleka alilieleza Mwananchi kuwa mahakama hiyo ilitoa hati ya wito huo Februari 8, mwaka huu.
Mahakama imetoa wito huo zaidi ya mwezi mmoja na nusu tangu ilipotoa uamuzi wa kukubali kufanya uchunguzi wa mwili wa marehemu.
Uamuzi wa kufanya uchunguzi ulitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga Desemba 19, 2022 kutokana na shauri la maombi namba 3 la mwaka 2022 lililofunguliwa na shemeji wa marehemu, Emmanuel Kagongo, kwa niaba ya familia ya marehemu.
Stella alifariki dunia usiku wa kuamkia Desemba 20 2020 akiwa mahabusu ya kituo cha Polisi Mburahati alikojisalimisha baada ya kupata taarifa kuwa alihitajika kituoni hapo.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni ilieleza Stella alijinyonga, lakini familia haikukubaliana na maelezo hayo badala yake ikaomba ufanyike uchunguzi huru kujua chanzo cha kifo chake, bila mafanikio.
Miaka miwili baada ya mwili kuzikwa, familia ikaenda mahakamani kufungua maombi hayo ya uchunguzi wa chanzo cha kifo hicho.
Wadaiwa katika shauri hilo ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspector General of Police - IGP), Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam (DZPC) na Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RPC).
Wengine ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Mburahati (OCD), mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), iliyofanya uchunguzi wa kitabibu wa chanzo cha kifo cha marehemu, lakini haikuwahi kutoa taarifa ya matokeo ya uchunguzi huo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Akizungumzia utaratibu wa uchunguzi huo, wakili Madeleka alisema pamoja na mambo mengine mahakama itatembelea maeneo yanayohusiana na tukio la kifo hicho na kuwauliza wahusika maswali mbalimbali.
Aliyataja maeneo hayo kuwa ni makaburini kwenye kaburi alikozikwa marehemu na mahabusu alikodaiwa kujinyonga.
Kituoni hapo, wakili Madeleka alisema mahakama itataka kujua kutoka kwa askari waliokuwa zamu wakishughulika na mapokezi na hifadhi ya mahabusu ni kwa namna gani walitimiza wajibu wao na kuona mazingira yanayoweza kumfanya mahabusu ajinyonge.
Pia Madeleka alisema mahakama itakwenda Muhimbili ambako mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi wa kitabibu wa chanzo cha kifo hicho, kuona ni namna gani waliendesha uchunguzi wao.
Awali wakati akitoa uamuzi wa kukubali maombi ya kufanya uchunguzi huo, Hakimu Kiswaga alisema kutokana na hoja za mwombaji na viapo kinzani vya wajibu maombi watatu hakuna ubishi kuwa Stella alifariki dunia katika mazingira tata akiwa katika kituo Cha Polisi Mburahati.
Alisema kwa kuwa wajibu maombi hususan Polisi hawakutekeleza wajibu wao wa kisheria yaani kutoa taarifa na hakuna taarifa zozote za uchunguzi uliofanyika kuonyesha chanzo cha kifo hicho, zilizowasilishwa mahakamani, basi mahakama hiyo ina jukumu la kuamuru ufanyike uchunguzi huo.
“Hivyo mahakama hii inaamuru ufanyike uchunguzi wa kifo cha Stella Moses ambaye mahakama inaona kwamba alifariki unnatural death (kifo kisicho cha asili) akiwa chini ya Jeshi la Polisi Mburahati, Desemba 20, 2020,”alisema Hakimu Kiswaga.