Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama Tanzania yadaiwa ‘chaka’

94654 Mahakama+pic Mahakama Tanzania yadaiwa ‘chaka’

Thu, 6 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Musoma. Mahakama mkoani Mara zinadaiwa kutumika kutakatisha fedha kwa kuwapatia ushindi wakopeshaji wanaofanya shughuli hiyo kinyume cha sheria.

Akizungumza mjini hapa juzi, mkuu wa Takukuru mkoa wa Mara, Alex Kuhanda alisema muda mrefu taasisi yake imeamua kupambana na wakopeshaji hao wanaotoza riba kubwa kinyume cha sheria huku wakiwalenga watumishi wastaafu hususan walimu.

Kuhanda alisema baada ya kugundua mbinu hizo waliamua kufanya uchunguzi na kubaini kuwapo kwa zaidi ya mashauri 80 yaliyofunguliwa mahakamani hususan za mwanzo na tayari wakopeshaji wamepewa ushindi.

“Tumebaini kuwa hawa wakopeshaji wanatumia mahakama kama kichaka cha kutakatisha fedha hii mbinu imewasaidia kwani kuna takwimu za kesi zilizofunguliwa katika mahakama zetu hasa za mwanzo na hawa wakopeshaji baadhi yao wamewapewa ushindi,” alisema.

Alitoa mfano mkopeshaji mmoja aliyefungua kesi 41 akidai kuwakopesha walimu 41 huku akiiomba mahakama kuamuru wadeni wake wamlipe Sh192.92 milioni sawa na asilimia 245 baada ya kuwakopesha walimu hao Sh52.92 milioni, kiwango ambacho ni kikubwa kwa ziada ya Sh129.82 milioni.

Akizungumzia madai hayo, hakimu mfawidhi mkoa wa Mara, Rahim Mushi alisema wamekubaliana Takukuru kufanya semina kwa mahakimu wote hususan za mwanzo kuwajengea uelewa juu ya suala hilo.

Pia Soma

Advertisement
Hata hivyo, Mushi alisema wakopeshaji hao wamekuwa wakiwasilisha mahakamani nyaraka mbalimbali juu ya madai yao ila hazionyeshi riba na Mahakama zimekuwa zikiingia mtego huo bila kujua.

Katika hatua nyingine, Takukuru inawashikilia viongozi wanane wa vyama vya msingi vya wakulima (Amcos) kwa tuhuma za ufujaji wa zaidi ya Sh18.8 milioni za wakulima kinyume cha sheria.

Viongozi hao ni wa Amcos mbili za Nyamatare ambayo viongozi wake wanadaiwa kufuja zaidi ya Sh13.2 milioni na Chaume Sh5.6 vyote vya wilaya ya Serengeti mkoani Mara ambao kwa pamoja wanadaiwa kufuja fedha hizo za wakulima wa pamba msimu wa 2019.

Chanzo: mwananchi.co.tz