Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama Iringa kusikiliza kesi ya ving’amuzi

16679 Pic+vinga TanzaniaWeb

Tue, 11 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iringa. Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imekubali kusikiliza maombi ya kupinga amri ya kuondolewa chaneli za ndani kwenye ving’amuzi vya Azam, Dstv, Zuku na Star Times.

Akitoa uamuzi huo Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Penterine Kente amesema Mahakama haioni sababu ya kukubaliana na mapingamizi yaliyowekwa na mwanasheria wa Serikali, Mwinyiheri Aristaric aliyeiomba itupilie mbali maombi hayo yaliyoletwa na watu watano kwa niaba ya watumiaji wa ving’amuzi hivyo.

Jaji Kente akitoa uamuzi huo leo Septemba 10,2018 ameeleza hoja zilizoletwa na wakili wa serikali ikiwemo kuomba Mahakama kutupilia mbali maombi hayo kwa kuwa muda wa siku 14 unaoitaka Mahakama kuanza kuyasikiliza umeshapita hakubaliani nayo.

Kwa sababu hoja hiyo imejaribu kushawishi Mahakama kuwabebesha mzigo waleta maombi ambao wao waliyaleta ndani ya muda kisheria.

Katika ombi lingine la wakili wa Serikali kuomba Mahakama kutupilia mbali maombi hayo akidai waleta maombi wameshindwa kuainisha kifungu cha sheria kilichowaongoza waleta maombi kuleta maombi hayo.

Jaji Kente amesema Mahakama inakubaliana na kifungu cha 19 cha Law reform (fatal accidents) miscellaneous provisions Act sura 310 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002 pamoja na kifungu kidogo cha 5(1) cha Law reform (fatal accidents and miscellaneous provisions)(judicial review procedure and fees) rules za 2014  kilichoainishwa na waleta maombi kwa kuwa mwanasheria wa Serikali licha ya kupinga kifungu hicho alishindwa kuainisha kifungu mbadala cha sheria ambacho waleta maombi walipaswa kunitumia.

Kutokana na maelezo hayo, Jaji Kente amesema Mahakama inatoa ruhusa kwa waleta maombi kuleta mahakamani maombi ya msingi ili Mahakama iweze kuyasikiliza na kutolea uamuzi.

Akizungumza nje ya Mahakama mara baada ya uamuzi huo, mmoja wa waleta maombi Oliver Motto amesema wamefurahishwa na uamuzi huo wa Mahakama na wanaamini Mahakama itatenda haki katika kusikiliza na kutoa uamuzi wa maombi hayo.

"Sisi kama walalamikaji tunafurahi Mahakama kukubali kusikiliza malalamiko yetu tukiwa na hoja za msingi ambazo tutaziwasilisha kupitia wakili wetu na tuna imani Mahakama itatenda haki," amesema. 

 

Wakili wa upande wa waleta maombi Chance Luwoga amesema wanakwenda kupeleka maombi hayo ya msingi sasa ili kuiwezesha Mahakama kutoa hukumu ya haki katika maombi hayo .

 

"Mahakama imetupa ruksa ya kupeleka maombi ya msingi ili iyasikilize kama vifungu vya sheria vinavyotutaka ili iyafanyie maamuzi" amesema Luwoga

 

Soma Zaidi: Mahakama yatupa mapingamizi ya Serikali ving’amuzi chaneli za ndani

 

Chanzo: mwananchi.co.tz