Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahabusu wamkimbia Zumaridi Gerezani

Zumaridi1 Pic Mhubiri Diana Bundala maarufu ‘Mfalme Zumaridi’

Sat, 18 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mhubiri Diana Bundala maarufu ‘Mfalme Zumaridi’ amefichua alipokuwa gerezani mahabusu wenzake walikuwa wanamuogopa hata muda mwingine wakimuona wanakimbia bila kujua sababu za wao kufanya hivyo.

Zumaridi amefichua hayo leo Jumamosi, Februari 18, 2023 akiwa nyumbani kwake akifurahia na waumini wake baada ya kuachiwa huru katika Gereza la Butimba jijini Mwanza kufuatia kesi tatu zilizokuwa zinamkabili ikiwemo ya usafirishaji haramu wa binadamu ambayo haina dhamana.

"Niliingia kwenye maombi nikamwambia Mungu abadilishe uongozi wa gereza hilo kwa sababu niliona nitafia humo, niliomba ili wanipunguzie adhabu kwa sababu nilikuwa hata nikimsalimia mahabusu mwenzangu wananikimbia bila kujua sababu," amesema Zumaridi.

Mhubiri huyo alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza baada ya kumkuta na hatia ya kuzuia maofisa wa Serikali kutekeleza majukumu yao katika kesi ya jinai namba 11 huku Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) akimfutia mashtaka katika kesi namba 10 na 12.

Katika kesi namba 11/2022, Zumaridi peke yake alikuwa anashtakiwa kwa kosa la usafirishaji haramu wa binadamu huku katika kesi namba 12, Zumaridi na wenzake 83 wakishtakiwa kwa kosa kufanya kusanyiko lisilo halali ambapo mashtaka yote yalifutwa na DPP baada ya kudai hana nia ya kuendelea na hizo.

Akizungumza leo nyumbani kwake, Mtaa wa Buguku, Kata ya Buhongwa jijini Mwanza, Zumaridi amesema alianza kuwa na imani kuwa maisha yake yatakuwa gerezani baada ya upande wa Jamhuri katika kesi mbili kati ya tatu, kutokamilisha upelelezi kwa wakati.

"Nilikuwa najua nimeshakuwa wa magereza maana kama mlivyokuwa mnasikia kila mara wanasema upelelezi bado, nikajua upelelezi unaweza kwenda hadi huko mbeleni, najisikia vizuri sana na namshukuru Mungu kwa kiwango cha juu kwa jinsi ninavyojisikia kuwa huru leo," amesema.

Pia, amesema sasa nafsi yake ina amani kwa kujumuika na familia yake baada kuwa mbali nayo kwa zaidi ya miezi 11, huku akisema anajipanga kuendelea na utoaji wa huduma za ibada.

"Natoa shukrani kwa kutoka salama, ugonjwa niliokuwa naumwa nimepima, lakini Mkuu wa Magereza (RPO) amenitoa maumivu yote niliyokuwa nayo kwa sababu nilipokuwa natumikia kifungo alinitaka kuwa mvumilivu hadi nitakapokimaliza niwe huru hatimaye leo niko huru," amesema Zumaridi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live