Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magufuli kuanza ziara Dodoma leo

Sun, 22 Apr 2018 Chanzo: habarileo.co.tz

RAIS John Magufuli leo anaanza ziara ya siku sita mkoani Dodoma ambayo pamoja na mambo mengine atalihutubia Bunge la Afrika Mashariki (EALA) linaloendelea vikao vyake mjini hapa.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amewaeleza waandishi wa habari kuwa, Rais Magufuli leo atawasili kuanza ziara hiyo.

Dk Mahenge amesema, Rais Magufuli atalihutubia Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Aprili 24, mwaka huu, ambalo kwa mara ya kwanza linafanyia vikao vyake mkoani Dodoma chini ya Spika wake, Martin Ngoga.

Kesho Jumatatu, atazindua jengo la Kitega Uchumi la Mfuko wa PSPF pamoja na Tawi la NMB la Kambarage ambalo lipo katika jengo hilo muhimu mjini humo.

Dk Mahenge amesema, Rais Magufuli pia atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zitakazofanyika kitaifa Aprili 26, mwaka huu kwenye uwanja wa Jamuhuri.

Mkuu wa mkoa amewataka wananchi watumie fursa ya maadhimisho hayo ya miaka 54 ya Muungano kufika kwa wingi kwenye huo kushuhudia maadhimisho hayo.

Ziara ya Rais Magufuli mkoani Dodoma itahitimishwa Aprili 27, mwaka huu kwa kufungua barabara ya Dodoma-Babati yenye urefu wa kilometa 231.8.

Chanzo: habarileo.co.tz