Mwanza. Rais wa Tanzania, John Magufuli amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kuhakikisha ujenzi wa wodi ya wanaume katika hospitali ya Wilaya ya Nyamagana Butimba jijini Mwanza unakamilika ifikapo Julai 30, 2019.
Jengo hilo la ghorofa mbili litagharimu zaidi ya Sh500 milioni likiwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 1000, ujenzi wake ulianza 2018.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Jumanne Julai 16, 2019 aliposimama kuwasalimia wananchi waliokusanyika kumuona karibu na hospitali hiyo wakati akitoka katika Gereza Kuu la Butimba Mwanza.
Ametoa maagizo hayo baada ya kutoridhishwa na majibu ya mkurugenzi mtendaji wa jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba na Mongella..
Rais alimkatisha Mongella wakati akitoa ufafanuzi kuhusu kukwama kwa mradi huo,“Mkuu wa mkoa simamia jambo hili, wajenge usiku na mchana nataka Julai 30, 2019 liwe limekamilika.”
“Na wewe (mkuu wa mkoa) utakuja mwenyewe kulifungua na ukifika hapa unanipigia simu. Unajua hatuwezi kuwachezea wananchi kiasi hiki jengo moja linajengwa mwaka mzima.”
Habari zinazohusiana na hii
- Idadi ya gunia za mchele kwa wafungwa yamshtua Magufuli
- Rais Magufuli: Mimi ni kama mfungwa mtarajiwa
- Rais Magufuli: Serikali haipendi watu wafungwe