Taarifa zilizotufikia kwenye dawati la habari zinaeleza kuwa, hali ni mbaya kwenye Stendi Kuu ya Mabasi Dar es Salaam iliyopo Mbezi Luis maarufu kama Magufuli Terminal hakuna huduma ya maji kwa muda wa siku tatu sasa.
Kwa mujibu wa abiria wa stendi hiyo, inadaiwa kuwa, kuanzia juzi Machi 26, 2023 hadi leo asubuhi ya Machi 28, 2023, hakuna maji na huduma ya vyoo imefungwa kutokana na kukosekana kwa maji.
Meneja wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Isihaka Waziri amesema; “Ni kweli tumepata changamoto kidogo, DAWASA hawana maji tangu Ijumaa kutokana na marekebisho ambayo wanafanya Ruvu Juu na Ruvu Chini.
“Hivyo tukawa tunatumia maj ya akiba ambayo nayo yametuishia, DAWASA waahidi kutuletea maji jana (Machi 27, 2023) lakini wakiwa njiani napo wakajulishwa kuwa Mloganzila hakuna maji, ikabidi wayapeleke huko.
“Usiku wa saa saba tukapata maji, lakini bahati mbaya pampu yetu nayo ikaharibika, hivyo mafundi wanaendelea kama kawaida.
“Huduma ya vyoo eneo la chini zimesimama kwa kuwa marekebisho yanaendelea. DAWASA wamesema baadaye maji yanaweza kuwa yamerejea,” alisema Isihaka.