Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magari yaliyokwama Mwanza yaanza safari

Mabasi Safariiiiii.jpeg Magari yaliyokwama Mwanza yaanza safari

Fri, 15 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Magari zaidi ya 200 yaliyokwama kutokana na kukatika barabara ya Kamanga-Sengerema mkoani Mwanza, eneo la Kijiji cha Igalagalilo iliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha jana Alhamisi Desemba 14, 2023 yameanza safari baada ya huduma kurejea.

Magari hayo yalikuwa yakitoa Mwanza kwenda Sengerema na mikoa ya jirani ya Geita, Kigoma na Kagera na kutoka maeneo hayo kwenda jijini humo.

Kutokana na hali hiyo, maofisa wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mwanza na Mbunge wa Sengerema (CCM), Hamis Tabasamu waliweka kambi eneo hilo, ili kuhakisha huduma zinarejea na magari yanaendelea na safari.

Tabasamu amesema wametumia zaidi ya saa 15 kurejesha mawasiliano hayo, huku wakishirikiana na Tanroads ambao waliweka kambi hadi saa tano usiku kusaidia abiria na magari yaliyokwama, ili waendelee na safari.

"Jitihada zimefanywa na meneja wa Tanroad akishirikiana na wananchi, wametumia saa 15 kujeresha huduma ya barabara hiyo,” amesema Tabasamu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Sengerema, Yanga Makaga amesema baada ya jitihada zilizofanywa huduma zimerejea, magari yameanza kupita na kuendelea na safari.

Ameiomba Serikali kujenga barabara hiyo ya vumbi kwa kiwango cha lami, ili kuondoa adha hiyo kwa wananchi.

"Suluhisho ya barabara hii ni kujengwa kwa kiwango cha lami, ili kuondoa adha ya kufanya ukarabati wa mara kwa mara,” amesema Makaga.

Juma Amos, Mkazi wa Kijiji cha Igalagalo amesema eneo hilo huwa ni korofi muda wote, hivyo Serikali inatakiwa kuhakisha wanafanya juu chini kukarabati eneo hilo ili lipitike muda wote.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live