Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magari makubwa kubeba abiria Mwanza

41859 SUMATRA+PIC Magari makubwa kubeba abiria Mwanza

Fri, 15 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra) mkoani hapa umetoa wito kwa wamiliki wa magari ya uchukuzi kufuata taratibu zilizowekwa, vinginevyo watafutiwa leseni.

Taratibu hizo ni pamoja na kuondoa magari madogo ‘hiace’ katikati mwa jiji  na kutoa wito wa kutuma maombi ya kupata leseni ya uchukuzi wa abiria kwa magari makubwa.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo, ofisa mfawidhi wa Sumatra mkoani Mwanza, Ngereza Patel amesema walitoa muda wa kutosha kwa wahusika kufanya maandalizi ya kuondoa magari madogo ya abiria na wengine kusajili magari yao makubwa.

Amesema zoezi la kuondoa na kusajili magari ya kubeba abiria lilianza Agosti 2018 na hadi kufikia Oktoba 2019 magari yasiyokidhi vigezo hayataruhusiwa kutumika katikati mwa jiji.

“Tunataka magari makubwa yenye uwezo wa kubeba abiria 25 na kuendelea yatoe huduma ya uchukuzi na wala sio ‘Hiace’. Hii itatusaidia kupunguza msongamano wa watu kwenye vituo vya magari hususan hapa jijini,” amesema Patel.

Amesema hawawezi kuziondoa ‘haice’ kwa wakati mmoja kwa kuwa hilo linaweza kusababisha changamoto kubwa kwa abiria hata kiuchumi. Muda wa mwaka mmoja unatosha kwa wahusika na wadau wengine kuzingatia taratibu za Sumatra.

“Tunafanya hivyo kwa awamu ili pia na abiria waweze kufahamu pale wanapoona magari makubwa  kama Coster yakiwa kituoni wasifikiri ni mabasi ya kwenda mikoani,” amesema.

 Patel amesema “Hiace’ zitakuwa zikitoa huduma ya usafiri nje ya jiji la Mwanza na tayari wameanza kutoa leseni za kufanya safari katika maeneno ya Kisesa-Kishiri hadi Nyashishi na Uwanja wa Ndege-Ilemela na Kisesa.

Mmoja kati ya wamiliki wa ‘Hiace’ jijini Mwanza, Othman Mohamed amesema utaratibu wa kuziondoa gari hizo utadumaza uchukuzi kwani kuna baadhi ya maeneo Coster haziwezi kupita kutokana na ufinyu wa maeneo.

“Kutoka pale stendi ya Nyasaka hadi stendi ya Igombe ni mbali mno na Coster haiwezi kupita pale au hata kupaki. Kwa kweli bado kutakuwa na changamoto kubwa,” amesema Mohamed.

Aidha baadhi ya wahudumu kwenye 'Hiace' wakiwamo makondakta wamesema magari hayo yameajiri watu wengi na iwapo zitaondolewa uwezekano wa wamiliki kuziegesha upo.

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz