Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magari madogo ya Moshi-Dar yapigwa vita

34488 Pic+magari Tanzania Web Photo

Wed, 2 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Baadhi ya wamiliki wa mabasi yaendayo jijini Dar es Salaam wameiomba Serikali kuangalia suala zima la utoaji vibali kwa magari madogo ya kubeba abiria kwenda masafa marefu Katika kipindi hiki ambapo kuna changamoto ya usafiri.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Januari 2, 2019, katika stendi kubwa ya mabasi Mjini Moshi, mmiliki wa magari ya Ibra Line, Ibrahim Shayo amesema magari hayo yaliyopewa vibali na Sumatra kusafirisha abiria kwa masafa marefu hayana viwango.

"Haya magari ya coaster, kiukweli yanachosha abiria kwa sababu mtu anakua amekaa kwa kujikunja, yaani anakua hayuko huru, Sumatra waangalie sana jambo hili japo yamesaidia kuondoa changamoto ya usafiri," amesema Shayo.

"Suala la usafirishaji wa abiria ni jambo nyeti lakini kumwambia abiria akae kwenye siti kama kigoda hatendewi haki, ingekuwa ni hivyo hata sisi wa magari makubwa tungeacha kununua magari ya gharama kubwa na kununua coaster lakini tunatambua hazifai kwa masafa marefu," amesema Shayo.

Katika kituo hicho, Mwananchi imeshuhudia adha ambayo wananchi wanaipata kutokana na wingi wa abiria kituoni hapo ukilinganishwa na magari yaliyopo na idadi kubwa ni wale wanaokwenda Dar es Salaam.

Naye Ofisa Mfawidhi, Sumatra mkoani hapa, Johns Makwale amesema wamelazimika kutoa vibali kwa magari hayo madogo kutokana na changamoto kubwa ambayo imekua ikijitokeza ya abiria kukosa usafiri.

"Japo watu wanalalamika lakini uwepo wa coaster hizi hapa stendi umesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto ya msongamano wa watu na ndio maana tunashuhudia changamoto ya usafiri si kubwa kama miaka mingine," amesema Makwale.

Jonathan Ndimba ambaye ni mmoja wa abiria amesema, wamelazimika kupanda gari hizo ndogo kwa kuwa hakuna magari makubwa.

"Hatuna namna, hapa stendi watu ni wengi mno, japo wamepandisha nauli hadi Sh30,000 imetulazimu tupande tu hivyo maana kadri muda unavyoenda magari yanajaa," amesema Ndimba.



Chanzo: mwananchi.co.tz