Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mafuta yaadimika Katavi

Mafuta Ers Mafuta yaadimika Katavi

Mon, 31 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shughuli za usafirishaji wa abiria kupitia usafiri wa pikipiki na bajaji mkoani Katavi zimesimama kutokana na ukosefu wa mafuta ya petrol na dizeli kwenye vituo vya kuuzia mafuta, hali iliyowaathiri madereva wa vyombo hivyo kukosa mahitaji ya familia zao.

Wakizungumza na mwananchi leo jana, Julai 30, 2023 baadhi ya madereva wa pikipiki na bajaji katika Manispaa ya Mpanda, wamesema zaidi ya siku nne sasa wamekumbwa na kadhia hiyo.

Dereva gari binafsi Masanja Salaganda, amesema kwasasa inawalazimu kupata mgawo wa lita moja moja ya mafuta kutokana na uhaba uliopo ili kila mwendesha chombo cha moto apate ambapo hayakidhi mahitaji.

“Tunajiuliza shida iko wapi labda kuna matatizo kati ya Serikali na wauza mafuta tunaumia sisi watumiaji, tunachoomba Serikali ilitatue suala hili kama dharura,” amesema.

John Shija dereva bajaji amesema takribani siku mbili amezunguka Mpanda nzima vituo vyote hakuna mafuta petrol na dizel na badala yake wananunua ya mgao.

“Unapewa bajaji bosi anataka Sh20,000 jioni kwa siku lakini tunashinda sheli kusubiri mafuta tunatoka saa nane, tunarundika madeni maana fedha ya kupeleka kwa bosi haifikii kwa siku," amesema na kuongeza;

“Tutaishije na familia wakati kula yetu ni sheli watoto wanalala njaa kwasababu shughuli zote zimesimama imepelekea bei kupanda, abiria sehemu ya kulipia Sh1000 wanalipa Sh3000,”

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Madema Ernest Madema, ambaye pia ni mmiliki wa kituo cha kuuzia mafuta cha Mwanone amekiri kuwepo hali hiyo akidai imemlazimu kuomba mafuta kutoka bohari za Serikali.

“Kweli changamoto ilikuwepo inatokana na uhitaji mkubwa, lakini mafuta tumepata imenibidi kuchukua kwenye bohari za Serikali mpaka sasa nimepakia magari manne.

“Mawili yameshaingia, moja liliingia jana usiku, lingine sasa hivi na kesho yataingia mengine mawili hivyo tatizo hili litaisha shida ilikuwa huko Dar es Salaam,” amesema.

Sanjari na hayo hali hiyo pia imesababisha bei ya usafiri kupanda kutoka Sh1000 kwa bajaji na pikipiki hadi kufikia Sh3000 huku wengine wakipaki vyombo vyao na abiria wakiathirika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live