Mvua iliyonyesha kwa zaidi ya saa tano katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza, imesababisha mafuriko eneo la Mkuyuni, wilaya ya Nyamagana.
Pia imesababisha shughuli za usafiri kusitishwa kwa zaidi ya saa tatu, huku baadhi ya waendesha pikipiki wakinusurika kusombwa na mafuriko hayo.
Nipashe ilifika katika eneo la tukio na kushuhudia adha walizokuwa wakizipata wasafiri waliokuwa wakienda katika shughuli zao, huku wengine wakilazimika kuteremka kwenye daladala na kubebwa mgongoni na baadhi ya vijana waliowatoza Sh. 500 ili kuvushwa eneo hilo.
Kadhalika, askari wa usalama barabarani waliwahi katika eneo hilo na kuanza kutoa mwongozo kwa waendesha vyombo vya moto kwa kuwaelekeza maeneo salama ya kupita.
Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya wananchi waliokumbwa na adha hiyo, waliiomba serikali kujenga upya daraja hilo kutokana na kuwapo kwa mafuriko ya aina hiyo kila msimu wa mvua, ambayo yanaathiri makazi na maduka.
Mmoja wa wakazi hao, Allan Abel alisema: “Hali hii imekuwa ya kila mwaka sasa mvua ikinyesha lazima maji yajae na hii inasababishwa na daraja hili kuwa finyu licha ya kuwa daraja linalounganisha barabara iendayo mikoani.”
Anna Hamisi, mmoja wa wasafiri waliokuwa wakiwahi mabasi yaendayo mikoani alisema kutokana na kadhia hiyo alishindwa kusafiri kuelekea msibani ambako alikuwa akiwahi basi na muda wake wa kuondoka ukawa umepita.
Baadhi ya vijana waliokuwa wakiwavusha wananchi wakiwamo madereva pikipiki walisema kadhia hiyo kwao imekuwa baraka kutokana na baadhi yao kupata zaidi ya Sh. 15,000 kwa muda mfupi.
Mmoja wa madereva hao, Revocutus Shabani, alisema: “Kwa muda huu tu nimebeba zaidi ya watu 15 licha ya kuwa hali ya kuvuka daraja hilo haikuwa nzuri, tulikuwa tukisaidiwa na askari wa usalama barabarani.”
Akizungumza kwa njia ya simu kuhusu utatuzi wa mafuriko katika daraja hilo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Paschal Ambrose, alisema daraja hilo si tatizo la mafuriko hayo. Alisema tatizo la mafuriko ni wananchi kutupa taka ovyo katika mitaro.
Alisema Halmashauri ya Jiji hilo inatakiwa kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya kutupa taka ili kudhibiti vitendo hivyo.