Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mafuriko yasomba reli, usafiri wa treni Morogoro- Dodoma wasitishwa

94501 Pic+mafyuriko Mafuriko yasomba reli, usafiri wa treni Morogoro- Dodoma wasitishwa

Wed, 5 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shirika la Reli nchini (TRC) limesitisha safari za treni kati ya Morogoro na Dodoma, kipande chenye cha urefu wa kilomita 120 kwa maelezo kuwa reli hiyo imeharibika.

Limeeleza kuwa usafiri huo utarejea baada ya siku 7 hadi 10 endapo mvua zinazoendelea kunyesha zitasimama ili kuruhusu ukarabati wa kipande kilichoathiriwa na mvua hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Februari 5, 2020 jijini Dar es Salaam, mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa amesema tayari shirika hilo limeanza kazi ya kuhamisha reli katika maeneo ambayo tuta la reli limesombwa na maji.

Kadogosa amesema takribani maeneo 26 yameathiriwa na mvua, ameyataja baadhi kuwa ni Kilosa (Morogoro), Gulwe (Mpwapwa), Igandu, Zuzu na Matukupora.

"Kwa sasa tunafanya juhudi za kuhamisha reli iwe mlimani zaidi, isifuate mto. Reli yote iliyoharibiwa, kilomita 120 itahamishwa kuwekwa mlimani," amesema Kadogosa.

Mkurugenzi huyo amebainisha kwamba baadhi ya abiria waliokuwa safarini walitafutiwa usafiri wa mabasi kumalizia safari yao huku wengine ambao walikuwa wasafiri jana wakirudishiwa nauli zao ili watafute usafiri mwingine.

Pia Soma

Advertisement
Hata hivyo, Kadogosa amesema reli za Dar - Kilimanjaro, Dar - Tanga na Mpanda - Tabora - Mwanza zinaendelea kutoa huduma kama kawaida kwa kusafirisha mizigo na abiria.

"Tunaangalia uwezekano wa kuendelea na huduma kuanzia Dodoma kwenda maeneo mengine kama Kigoma na Mwanza," amesema Kadogosa na kubainisha kwamba historia inaonyesha kuwa kila baada ya miaka 10, mvua kubwa huathiri miundombinu ya reli.

Chanzo: mwananchi.co.tz