Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mafuriko yamnyang’anya mama mtoto mkononi

80860 Pic+mafuriko Mafuriko yamnyang’anya mama mtoto mkononi

Mon, 21 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

MwanzaWakati mtoto mwenye umri wa miaka mitatu anahofiwa kufa kwa kusombwa na maji, watu wawili wamenusurika kufa kutokana mafuriko yalitokana na mvua iliyonyesha jijini Mwanza jana Ijumaa mchana Oktoba 18, 2019.

Mvua hiyo iliyonyesha kwa zaidi ya saa moja mchana kuanzia saa 7:45 mchana hadi saa 9:14 alasiri pia ilisababisha mto Mirongo inayopita katikati ya jiji kufurika na kusomba bidhaa zilizopangwa kwenye mabaraza ya maduka ya jumla na rejereja katika mitaa ya Liberty na Uhuru jijini humo.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu akiwa eneo la tukio kuongoza juhudi za uokoaji, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Igogo, Shadrack Mboje alisema mtoto anayehofiwa kufariki alikwapuliwa kutoka mikononi mwa mama yake aliyezidiwa na nguvu ya maji alipokuwa akijaribu kujiokoa akiwa na watoto wake wawili.

“Yule mama alilazimika kujaribu kujiokoa akiwa na watoto wake wawili baada ya nyumba yao kubomolewa na mafuriko; alikuwa amembeba mtoto mdogo huku mkubwa akiwa amemshikilia mkono ndipo alipomzidi nguvu ya maji yaliyomsomba mtoto mkubwa,” alisema Mboje

“Amebaki na mtoto mdogo aliyekuwa amembeba mkononi baada ya juhudi zake za kumwokoa mtoto wake mkubwa kushindikana kutokana na kasi ya maji,” aliongeza

Ofisa mtendaji huyo alisema juhudi zilikuwa zikiendelea kumtafuta mtoto aliyesombwa na maji ambaye hadi saa 11:00 jioni jana alikuwa hajapatikana.

Pia Soma

Advertisement
Katika tukio lingine; bidhaa za wafanyabiashara wa maduka ya jumla na rejereja katika mitaa ya Liberty na Uhuru zilisombwa na maji ya mto Mirongo iliyojaa na kusambaa mitaani huku daraja likiwa limefunikwa.

Miongoni mwa bidhaa zilizosombwa na maji ya mto huo unaomwaga maji yake ndani ya Ziwa Victoria ni pamoja mabeseni, ndoo, malapa/yeboyebo na madumu ya mafuta ya kupikia.

Kusombwa kwa bidhaa hizo nusura kusababishe kifo cha Salvatory Wandalu aliyesurika kufa maji alipokuwa akijaribu kuokoa mapipa tupu yaliyokuwa yakisombwa.

Kunusurika kwa Salvatory kulitokana na jitihada binafsi za Simon Ally aliyejitoa mhanga na kujitosa ndani ya maji kumwokoa mwenzake huku umati uliokuwa ukishuhudia tukio hilo ukipiga kelele za kuomba msaada.

Mto Mirongo inayokatisha katikati ya jiji la Mwanza hukusanya maji yake kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya za Nyamagana, Ilemela, Magu na Misungwi.

Kwa wilaya ya Nyamagana, maji yam to huo yanatoka maeneo ya Igoma, Mabatini na Kishili kwa Jiji la Mwanza huku maji mengine wakati kwa kwa Magu maji hayo hutokea maeneo ya Kisesa.

Wafanyabiashara wa soko kuu la muda jijini Mwanza eneo la Mbugani nao wameonja adha ya mvua hizo baada ya bidhaa zao kuharibiwa na maji ya mvua kutokana na miundombinu ya soko hilo kushindwa kuhimili mvua nyingi zilizonyesha juzi na jana.

Walioathirika zaidi kutokana na paa za vibanda vya biashara sokoni hapo kuwa fupi na hivyo kusababisha maji kumwagikia kwenye meza walizopanga bidhaa ni wafanyabiashara wa nafaka akiwemo Eva Urassa anayeuza dengu, kunde, maharagwe, mchele na karanga.

Wakati Mkurugenzi wa jiji la Mwanza, Kilomoni Kibamba aliyetebelea soko hilo alimwagiza mkandarasi anayejenga vibanda na kuta za soko hilo kurekebisha kasoro zilizobainika ifikapo Jumatatu Oktoba 21, 2019, Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella aliahidi kuzungumzia madhara ya mvua zinazoendelea kunyesha baada ya kukusanya taarifa kutoka kwa viongozi na watendaji wa wilaya na halmashauri zote za mkoa huo.

Imeandikwa na Peter Saramba, Jesse Mikofu na Sada Amir

Chanzo: mwananchi.co.tz