Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mafuriko Tanga, gari yasombwa na maji

32436 Mafurikopic Tanzania Web Photo

Wed, 19 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanga. Baadhi ya nyumba katika mitaa ya Jiji laTanga zimejaa maji huku barabara kadhaa zikishindwa kupitika kufuatia mvua kubwa iliyoambatana na upepo kunyesha usiku wa kuamkia leo Jumatano Desemba 19, 2018.

Mwananchi limeshuhudia gari dogo aina ya Toyota IST likisombwa na maji huku baadhi ya nyumba katika mitaa ya Magomeni, Mikanjuni, Mwakidila na Neema zikizingirwa na maji huku wakazi wake wakishindwa kutoka nje.

Barabara kutoka kituo cha Afya Makorora kuelekea Usagara magari yalishindwa kupita ambako gari dogo aina ya Toyota IST likisombwa na maji.

Mawasiliano kati ya Tanga mjini na Wilaya ya Pangani yalikatika kwa muda kutokana na magari kukwama eneo la Neema kata ya Tangasisi.

Meya wa Jiji la Tanga, Mhina Mustapher  ‘Selebos’ alitembelea maeneo yaliyoathirika na mvua na kuahidi kuwasiliana  na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) kuhakikisha miundombinu inakarabatiwa na kurejea katika hali yake ya kawaida.

"Niwape pole walioathirika na mvua, ila nawaahidi kuwa nitawasiliana na wenzetu wa Tarura kuwaomba warekebishe miundombinu ili maji yaweze kupita kwa urahisi,” amesema Selebos.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz