Ikiwa ni siku chache tuu baada ya kukamatwa kwa watuhumiwa wa wizi wa simu za mkononi wengi wao wakiwa ni mafundi wa simu, Jeshi la Polisi mkoa Morogoro Julai 17, 2023 katika viwanja vya Bwalo la JKT Umwema Manispaa ya Morogoro limefanya kikao na mafundi simu kwa lengo la kushirikiana katika kutokomeza uhalifu wa wizi wa simu mkoani hapa.
Kikao hicho kiliongozwa na Mkuu wa oparesheni Mkoa Morogoro Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) LINUS MNYAMBWA ambapo amezungumza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwaasa na kuwaonya juu ya upokeaji wa simu za wizi kutoka kwa waporaji wanaotumia pikipiki maarufu kama Vishandu.
ACP Mnyambwa Aliwaeleza madhara ya kukamatwa na simu za wizi ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani na kupewa adhabu kali ambayo itapelekea kuyagharimu maisha yao.
Akiongea na mafundi simu hao Mkuu wa Upelelezi Mkoa Mrakibu wa Polisi (SP). Chrispin Lugalabam Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Morogoro aliwataka;
Kutoa taarifa za simu za wahalifu wanaokuja kuflash simu pindi wanapowatilia mashaka kuwa simu hizo huenda zikawa za wizi, kuacha kabisa kuwa wapokeaji wa simu za wizi, kuweka utaratiibu mzuri wa kuwaorodhesha wateja wao wanaokuja kutengeneza simu katika ofisi zao.
Kikao hicho kilihudhuliwa pia na Mkuu wa Upelelezi wilaya ya Morogoro, Mkuu wa operesheni wilaya, wakuu wa vitengo vya cyber mkoa na wilaya pamoja na askari wa cyber ambao walianzisha majadiliano juu ya namna bora ya kupambana na uhalifu huu wa wizi wa simu pamoja uhalifu mwingine.