Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), umetoa taarifa kwa Watumiaji wa kivuko cha MV. KILINDONI kinachotoa huduma kati ya Mafia Wilayani Mafia na Nyamisati Wilayani Rufiji Mkoani Pwani kuwa kivuko hicho hakijasafiri alfajiri ya leo kutokana na kupata hitilafu kwenye injini yake moja.
Taarifa iliyotolewa na TEMESA leo October 10,2024 imesema “Kwa mujibu wa ratiba, Kivuko MV. KILINDONI kilipaswa kuondoka alfajiri ya leo kutoka Bandari ya Mafia kuelekea Bandari ya Nyamisati lakini kitashindwa kuondoka kutokana na kupata hitilafu katika mifumo yake ya undeshaji ambayo imesababisha injini moja kushindwa kufanya kazi hivyo kivuko kubakia na injini moja pekee inayofanya kazi”
“Juhudi za kurekebisha changamoto zilizojitokeza katika kivuko MV. KILINDONI chenye uwezo wa kubeba tani 100, abiria 200 na magari 10 zinaendelea kufanywa na Mafundi wetu hadi wakati huu ili kukirejesha katika hali yake ya kawaida na kutokana na hitilafu hiyo, safari ya kutoka Mafia kwenda Nyamisati haitakuwepo siku ya leo”
“TEMESA inawaomba radhi abiria wote wanaotumia usafiri wa kivuko MV. KILINDONI kutokana na changamoto iliyojitokeza na inawakumbusha kuendelea kufuata maelekezo ya Mabaharia wakati wote wanapotumia vivuko ili kuendelea kuwa salama”