Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mafanikio ya elimu katikati ya changamoto lukuki Kilwa

E6ae60a9141e7a629dcfaa059044fa2a Mafanikio ya elimu katikati ya changamoto lukuki Kilwa

Mon, 20 Dec 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mkoa wa Lindi umepiga hatua kubwa katika kupunguza kiwango cha umasikini uliokithiri cha watu kuishi chini ya dola moja kwa siku.

Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) za mwaka 2016 zinaonesha kuwa mkoa huo kwa wastani wananchi wake wamevuka kiwango hicho.

Aidha, takwimu za mwaka 2009 pato lilikuwa Sh 767,948 na mwaka 2015 liliongezeka na kufikia Sh 1,901,044 ikiwa ni ongezeko la asilimia 148 kwa wastani wa ongezeko la asilimia 21 kwa mwaka.

Pia pato la mkoa limeen[1]delea kuongezeka kutoka Sh 695,361,000 mwaka 2009 hadi kufikia Sh 1,690,403,000 mwaka 2015, hili ni ongezeko la asilimia 143 kwa wastani wa asilimia 20 kwa mwaka.

Hata hivyo, katika tovuti ya mkoa imeelezwa kuwa pamoja na mafanikio hayo bado kuna changamoto kubwa ya umaskini na mimba za utotoni.

Moja ya wilaya yenye changamoto ni Kilwa na kutokana na tatizo hilo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, ilianzisha kampeni maalumu “Tuwasaidie Watoto Wasome, Wakue, Mimba baadae”.

Khajilu Bohi, Ofisa Elimu, Vifaa na Takwimu kutoka Kilwa aliiambia HabariLEO kuwa kwa mwaka 2020 katika kipindi cha likizo ya dharura ya corona watoto 106 walipata ujauzito.

Kutokana na hali hiyo walianzisha kampeni hiyo pamoja na msako wa wanafunzi wasioenda shule kumkamata mzazi na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Hii imesaidia, kwani takwimu za mwaka huu 2021 watoto 14 tu ndio wamekatiza masomo kwa ujauzito,” anasema Bohi.

Anasema changamoto ya umbali mrefu na wazazi kuachia jukumu la malezi kwa walimu ndio sababu ya mdondoko wa elimu kwenye wilaya hiyo kutokana na wasichana kusaka njia ya mkato kurahisisha maisha.

“Kwa jiografia ya wilaya yetu, mwanafunzi analazimika kutembea kilometa 10 mpaka 15 kwenda shule, hii ni changamoto ambayo inachangia watoto wa kike kuingia kwenye vishawishi kutokana na kipato duni cha wazazi ambao hawamudu gharama za kuwalipia nauli ya basi kila siku,” anasema Bohi.

Naye mzee maarufu wa Kilwa, aliyempa Rais John Magufuli jogoo Julai 30, mwaka jana (2020), Shaweri Mohammed maarufu ‘Kimbwembwe’ anasema mimba za utotoni nyingi katika Wilaya ya Kilwa na Mkoa wa Lindi kwa ujumla inatokana na asilimia kubwa ya vizazi havijaenda shule.

“Kwa kuwa tulikosa elimu ndio maana wazazi wengi hawaoni umuhimu wa kupeleka watoto shule, ukiangalia mfano mimi babu yangu hakusoma, mimi sikusoma, hivyo kuona umuhimu wa kumpeleka mtoto shule hamna, msimu wa shamba mtoto haendi shule anaenda kulinda ndege shambani, unyago anapelekwa kwenye unyago badala ya kwenda shule anakaa porini miezi mitatu anachezwa unyago masomo atakumbuka?” anahoji Mohammed.

Mzee Mohammed anashauri ili kumaliza tatizo hilo serikali ijenge shule za sekondari na bweni, watoto wa kike walale huko huko lakini kwa sasa mtoto anatembea kilometa 15 kwenda shule, na kurudi 15, kwa siku anatembea kilometa 30 hapo katikati kuna madereva wa malori, kuna bodaboda unadhani watawaacha salama?

“Mfano Kata ya Somanga mpaka sasa hamna shule ya sekondari, Shule ya Msingi Somanga inafaulisha watoto wengi zaidi ya 100 wanapelekwa Shule ya Sekondari Kinjumbi ambayo ipo kilometa 14 kutoka Somanga, kwenda na kurudi kila siku kilometa 28, huu umbali unachangia mdondoko wa elimu katika wilaya yetu,” anasema.

Mzee Mohammed anasema hata shule zilizopo hazikithi viwango, anatolea mfano Shule ya Sekondari Mingumbi iliyo kwenye hali mbaya ya kukosa barabara ya kufika shule.

“Kipindi cha masika ni tabu, mwalimu inabidi avue viatu atembee peku, shule imechoka ina nyufa muda wowote inaanguka. Changamoto kubwa ni madarasa.”

SABABU ZA UTORO

Kwa mujibu wa utafiti wa kihabari uliofanywa na mwandishi wa makala haya, umebaini kuwa pamoja na sababu nyingine, mwamko mdogo wa elimu miongoni mwa wazazi na walezi ni sababu.

Pia, shughuli za uvuvi, kilimo, zinazowalazimisha baadhi ya wazazi na walezi kuishi mbali na familia, hivyo kuwaachia watoto jukumu la kujilea wenyewe.

“Huku Kilwa hasa Kata ya Mandawa kilimo chake ni cha kuhamahama na wanalima sana ufuta, mtama na mahindi, wazazi wanaweza kukaa shambani kwa muda mrefu, huku watoto wakibaki kujilea wenyewe.

“Mtoto mkubwa wa familia anayeachiwa jukumu la kuwalea wadogo zake anapokuwa wa kike hali huwa mbaya zaidi kwa sababu hukutana na vishawishi vinavyoweza kumfanya si tu awe mtoro, bali kupata ujauzito,” anasema Rashid Limba, Ofisa Mtendaji Kata ya Mandawa.

Anasema uhaba wa taulo za kike pia unachangia watoto kuacha shule na kujitumbuki[1]za katika biashara ya ngono katika umri mdogo ili aweze kukidhi mahitaji.

“Serikali kwa kushirikiana na wazazi na wadau wa maendeleo wamejenga hosteli katika baadhi ya kata, lakini baadhi ya wazazi hawapo tayari kuruhusu watoto wao kuishi bwenini kwa kuhofia kupunguza nguvu kazi nyumbani,” anasema Limba na kuongeza:

“Hata wale wazazi wanaowaruhusu watoto wao kuishi hosteli hawako tayari kuchangia maharagwe na mahindi kwa ajili ya chakula licha ya watoto wao kutembea umbali mrefu.

Hali hiyo huwalazimu baadhi ya wanafunzi kupanga na kuishi kwenye vyumba vya mitaani maarufu kama geto, ambako hakuna usimamizi wala uangalizi wa wazazi na walimu.

KILIO CHA WALIMU

Ofisa Elimu Msingi wa Wilaya, Hussein Kitingi, anasema wilaya hiyo ina shule za msingi 108 za serikali na tatu za binafsi na kufanya idadi ya shule 111.

Utoro na mimba ni kati ya changamoto zinazokwamisha maendeleo ya kitaaluma.

Anasema katika kipindi cha mwaka 2020 na 2021, jumla ya wanafunzi 139 waliopaswa kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu, hawajafanya kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito.

MWANAFUNZI ANENA

Idd Selemani (si majina halisi) ni miongoni mwa wanafunzi wa kidato cha pili anawasihi wazazi kutimiza wajibu wa malezi na maandalizi yao kwa ajili ya maisha ya baadaye

Chanzo: www.habarileo.co.tz