MADUKA 10 yaliyopo Kayanga mjini wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, yameteketea kwa moto.
Majengo hayo yanamilikiwa na familia ya Nekemia Kazimoto (Kazikomu) na yapo mkabala na majengo ya City Center na Magereza Kayanga.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Godfrey Mheluka, moto huo ulizuka saa 5 usiku katika duka moja la nguo na kusambaa maduka mengine ya bidhaa mbalimbali.
Alisema moto huo ulidumu zaidi saa nne na chanzo chake hakijafahamika.
“Hatufahamu chanzo kwani moto ulianza wakati umeme umezimika. Hakukuwa na umeme, hivyo ni ngumu sana kujua chanzo,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Alisema kamati ya maafa ya wilaya, itakutana leo kuchambua hasara iliyopatikana na kuangalia namna bora ya kurejesha eneo hilo katika hali yake ya kawaida.
Uwepo wa matukio ya moto katika maduka na masoko, ulisababisha wananchi kuhamasishana na kujenga ofisi ya zima moto, lakini bado ofisi hiyo haina vifaa vya kuzimia moto.
Mheluka alisema ofisi hiyo imekamilika lakini haina vifaa. Alisema halmashauri imepeleka maombi ya kupata gari la zima moto na Kamishina wa Zimamoto ameahidi kuwapatia gari mwakani.
Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wafanyabiashara kukagua mifumo ya umeme katika maduka yao, ili kuepukana na changamoto zinazojitokeza mara kwa mara