Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madiwani wazuia ujenzi duka la nyama Impala

36f9528d098fd2682f00ceb11d689a43.jpeg Madiwani wazuia ujenzi duka la nyama Impala

Mon, 15 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

BARAZA la madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, limesimamisha ujenzi wa duka la kuuza nyama ya ng'ombe na mbuzi kwenye eneo la wazi la mzunguko wa Impala.

Uamuzi huo ulifanywa mwishoni mwa wiki, baada ya madiwani kuhoji uhalali wa ujenzi wa duka hilo, lililotarajiwa kujengwa na Kampuni ya Arusha Meat, inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji hilo.

Meya, Maximilian Ilanghe, aliwaeleza madiwani kuwa ujenzi huo unasimamishwa mpaka taratibu zitakapofuatwa.

Madiwani hao walihoji uhalali wa ujenzi wa duka hilo, kwa maelezo kuwa kamati ya wataalamu wa halmashauri hiyo haikuzingatia taratibu za ujenzi.

Walisema kamati ya mipango miji na kamati ya fedha, hazikushirikishwa hivyo kamati hiyo ya wataalamu, haikuwa na mamlaka kuidhinisha ujenzi huo.

Madiwani walisema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alizua ujenzi kwenye eneo hilo na aliagiza libaki wazi kwa ajili ya watu kulitumia kwa mapumziko.

Walisema kama utafanyika ujenzi, basi lijengwe jengo la muda ambalo linaweza kuhamishwa wakati wowote na si kujenga jengo la kudumu.

Kaimu Mhandisi wa halmashauri hiyo, Samweli Mshuza, aliwaeleza madiwani kwamba mradi huo wa duka, unalenga kuiongezea mapato halmashauri kwa kuwa mradi ni kitega uchumi.

Meneja wa Kampuni ya Arusha Meat, Stephen Sultani, alilieleza baraza hilo kuwa kampuni hiyo inamilikiwa kwa asilimia 100 na halmashauri hiyo, hivyo kujengwa kwa duka hilo ni kusogeza huduma kwa wananchi

Alisema kabla ya kuanza ujenzi, kampuni hiyo iliwasiliana na ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo kwa ajili ya ujenzi huo.

Chanzo: habarileo.co.tz